Mashambulizi Idlib yaweka mbinyo makubalino ya Uturuki na EU
29 Desemba 2019Rais wa Uturuki Tayyip Erdogan ameonya kuwa makubaliano kuhusu wakimbizi na Umoja wa Ulaya yamo hatarini.
Kwa wiki kadhaa jimbo la Idlib nchini Syria , ngome ya mwisho iliyobaki ya waasi wa jihadi , limekuwa likishambuliwa kutoka majeshi ya serikali ya Syria na Urusi. Mashambulizi ya makombora , maroketi na mashambulizi ya angani yamesababisha miji mingi kuharibika. Kutokana na mashambulizi yanayoendelea , chama cha madaktari wa Marekani (SAMS), shirika linalotoa msaada wa matibabu, limefunga operesheni zake katika hospitali mbili za jimbo hilo.
Shirika la Medico International , shirika la kutoa misaada ya kiutu pamoja na haki za binadamu, limeripoti kuwa katika muda wa wiki kadha zilizopita , kiasi cha hospitali 100 zimeshambuliwa kwa makusudi kwa mabomu.
Kutokana na mashambulizi haya yanayoendelea, mamia kwa maelfu ya raia wamekimbia makaazi yao . Kwa mujibu wa kundi la urtibu la kuchukua hatua za kutoa misaada, kiasi ya watu 217,000 wamekimbia tangu Novemba mwaka huu.
Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan ameonya kuwa hatua mpya ya watu kukimbilia nchini humo kwa wingi , kama ilivyokuwa mwaka 2015, wakati idadi kubwa ya walioomba hifadhi waliingia katika mataifa ya Ulaya , huenda ikatokea.
Mamia wakimbia mashambulizi Syria
Amesema kampeni ya mashambulizi katika jimbo la Idlib tayari imesababisha watu 80,000 kukimbia kutoka jimbo hilo, ambao sasa wanaelekea Uturuki. Rais amesema nchi yake " haiwezi tena kubeba mzigo huo yenyewe," na kuongeza kuwa "Nchi zote za Ulaya , na hususan Ugiriki, zitakuja kupata athari zake" kutokana na watu wengi kukimbia nchi hiyo.
makubaliano na Umoja wa Ulaya yanaitaka Uturuki kuzuwia waomba hifadhi kuondoka kutoka katika ardhi yake kwenda katika visiwa vya karibu vya Ugiriki kwa msaada wa watu wanaosafirisha watu kwa njia haramu. Kwa upande wake Uturuki , hadi mwaka uliopita itapata kutoka Umoja wa Ulaya euro bilioni 6 kuimarisha hali ya maisha ya wakimbizi waliokimbilia Uturuki.
Makubaliano hayo pia yanalenga kuwa wahamiaji ambao hawana hadhi ya ukimbizi barani Ulaya watarejeshwa kutoka visiwa vya Ugiriki kwenda uturuki.
Umoja wa Ulaya pia umeahidi kuanza mazungumzo juu ya kuondoa mahitaji ya visa kwa raia wa Uturuki kwenda Ulaya na uwezekano wa Uturuki kuwa mwanachama wa Umoja huo.
Uturuki kwa sasa , inataka kujadili makubaliano yaliyopo hivi sasa kutokana na kuongezeka kwa idadi ya wakimbizi. Na mapema majira ya joto mwaka huu, Erdogan alitishia kuwaruhusu waomba hifadhi kusafiri kwenda Ulaya hadi pale Umoja huo utakapoongeza msaada wake wa kifedha kwa wakimbizi wanaoishi Uturuki. Hadi sasa Uturuki imewachukua wakimbizi wapatao milioni 3.6 kutoka Syria.