1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mashambulizi kwenye makanisa Kenya yauwa 19

1 Julai 2012

Watu wenye silaha wameyashambulia makanisa mawili kaskazini mashariki mwa Kenya, na kuuwa watu 19 huku wengine zaidi ya 40 wakijeruhiwa. Polisi imesema washukiwa saba wamehusika katika mashambulizi hayo.

Bendera ya Kenya
Bendera ya KenyaPicha: Fotolia/aaastocks

Kwa mujibu wa taarifa za shirika la Msalaba Mwekundu nchini humo, mashambulizi hayo yametokea kwa wakati mmoja waumini wakiwa katika ibada. Watu hao wasiojulikana na waliokuwa wamefunika nyuso zao waliwamiminia risasi waumini katika kanisa la kikatoliki na kanisa la Africa Inland Church AIC, mjini Garissa kaskazini mashariki mwa Kenya.

Naibu kamanda wa polisi katika eneo hilo Philip Ndolo, amesema washambuliaji hao waliwauwa maafisa wawili wa polisi na kuwanyang'anya bunduki zao kabla ya kuyavamia makanisa hayo.

''Hatujamkamata mshukiwa yeyote lakini tunazo taarifa kuwa watu watano walihusika katika mashambulizi yaliyofanywa kwenye kanisa la Africa Inland Church, wakitumia maguruneti na bunduki, huku wawili wengine wakihusika kwenye mauaji ndani ya kanisa katoliki.'' Philip Ndolo alikiambia kituo cha Radio cha huko Kenya, Capital FM.

Shirika la Msalaba Mwekundu limearifu kuwa majeruhi wasiopungua 10 wamelazwa katika hospitali ya mkoa wakiwa katika hali mahututi, sita miongoni mwao wakiwa wanawake.

Baraza la waislamu layalaani mashambulizi

Baraza kuu la waislamu nchini Kenya limeyalaani mara moja mauaji hayo, na kutuma salamu za rambirambi kwa familia zilizopoteza wapendwa wao.

Kambi ya wakimbizi ya Dabaab iko karibu na mji wa GarissaPicha: AP

Mji wa Garissa una wakazi wengi waislamu wenye asili ya kisomali, na uko karibu na kambi ya wakimbizi ya Dadaab na pia karibu na mpaka wa nchi ya Somalia ambayo inakabiliwa na machafuko kwa zaidi ya miongo miwili. Eneo uliko mji huo limekuwa lenye mivutano tangu Kenya ilipopeleka jeshi lake kusini mwa Somalia mwaka jana kupambana na waasi wa Al-Shabaab.

Mfululizo wa mashambulizi

Ijumaa iliyopita, washambuliaji waliuvamia msafara wa shirika la misaada kutoka Norway karibu na kambi ya wakimbizi ya Dabaab, wakamuuwa dereva wa gari na kuwachukua mateka watu sita wakiwemo raia wanne wa kigeni. Dabaab ndio kambi kubwa zaidi ya wakimbizi duniani.

Wanamgambo wa Al-Shabaab wamehusishwa na mashambulizi ndani ya KenyaPicha: picture-alliance/Photoshot

Mwaka jana wafanyakazi wawili wa shirika la msaada la madaktari wasio na mpaka, (Medicins sans Frontieres) MSF, walitekwa nyara na hadi leo hawajaachiwa huru. Inaaminika kuwa wamepelekwa kusini mwa Somalia, eneo ambalo bado liko mikononi mwa waasi wa al Shabaab, ambalo lina mafungamano na kundi la kigaidi la al-Qaida

Mwandishi: Daniel Gakuba/dpa

Mhariri: Amina Abubakar

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi