Mashambulizi makali ya angani yatikisa Khartoum tena
18 Mei 2023Mashambulizi makali ya angani yamerindima katika mji mkuu wa Sudan Khartoum leo, huku mapigano yakiongezeka karibu na kambi ya kijeshi.
Mashuhuda wameelezea hayo kuhusu machafuko ambayo tayari yamesababisha takriban watu milioni moja kuondoka Khartoum.
Kulingana na mashuhuda, mashambulizi ya angani yaliyolenga maneo ya wanamgambo wa Rapid Support (RSF) yamesikika katika mitaa kadhaa kusini mwa mji huo, ikiwemo karibu na kambi ya Taiba, wakati pia polisi wanaoshirikiana na jeshi wakipambana na wanamgambo.
Jeshi limekuwa likitumia zaidi operesheni ya angani na silaha nzito katika juhudi zake za kujaribu kuwasogeza nyuma wanamgambo wa RSF ambao wamekamata maeneo kadhaa ya Khartoum na miji Jirani ya Bahrin na Omdurman.
Machafuko hayo ya kung'ang'ania madaraka kati ya jeshi linaloongozwa na jenerali Abdel Fattah al-Burhan, na kikosi chenye nguvu cha wanamgambo RSF kinachoongozwa na Mohamed Hamdan Dagalo, yalianza Aprili 15.