1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroIran

Mashambulizi makubwa ya Israel yatikisa Tehran

5 Machi 2026

Israel imefanya mashambulizi makubwa mjini Tehran ikilenga kile ilichosema ni miundombinu ya mamlaka za Jamhuri hiyo ya Kiislamu ingawa Iran haijatoa maelezo ya kina kuhusu kiwango cha uharibifu.

Tehran | Iran 2026 | Mashambulizi ya anga ya Israel
Moshi ukifuka kufuata mashambulizi ya anga yaliyofanywa na Israel katika eneo la kaskazini-magharibi mwa TehranPicha: Fatemeh Bahrami/Anadolu/picture alliance

Waandishi wa shirika la habari la AFP walioko mjini Tehran wameripoti kuona ndege kadhaa za kivita zikipita angani upande wa Magharibi mwa mji mkuu huo na kusikia milipuko mikubwa.

Jeshi la Israel limesema mashambulizi yake ya hivi karibuni dhidi ya Iran "yameutikisa" uongozi wa kidini wa Jamhuri hiyo ya Kiislamu.

Msemaji wa jeshi la Israel Effie Defrin amesema, "Lengo la operesheni hiyo ni kusababisha uharibifu mkubwa ndani serikali ya kigaidi ya Iran hadi iondoe kitisho kilichopo - na tunaendelea kusababisha madhara kwa uongozi uliopo. Ni muhimu kwangu kusema kwamba tayari Iran imetikisika. Ilitikiswa na shambulio la kwanza Jumamosi asubuhi, wakati uongozi ulipoondolewa. Na kila siku tunaendelea kuudhoofisha zaidi hadi tishio liondoke."

Ama kwa upande mwingine, mapema leo mjini Jerusalem, milipuko imesikika baada ya onyo la shambulio la makombora, huku mamlaka ikiwaondoa haraka watu kutoka majumbani mwao na kuwapeleka maeneo salama.

Iran yajibu kwa makombora kuelekea Jerusalem

Maafisa wa huduma za dharura wa Israel wakifanya ukaguzi katika vifusi baada ya shambulio la kombora la Iran karibu na Bet Shemesh, takriban kilomita 30 magharibi mwa JerusalemPicha: Ahmad Gharabli/AFP

Kwingineko, Iran imewashambulia wapiganaji wa Kikurdi walioko nchini Iraq, ikiwatuhumu kupanga njama za kuingia Iran kisiri. Ripoti zinaeleza kuwa Marekani inadaiwa kuwapa silaha baadhi ya wapiganaji hao, jambo ambalo Tehran inaliona kama tishio kwa usalama wake wa ndani.

Katibu wa Baraza Kuu la Usalama la Iran, Ali Larijani, ametoa onyo kali kwa makundi hayo ya Kikurdi, akisema serikali itakabaliana nayo vikali.

Na nchini Lebanon, Israel imesema vikosi vyake vimevilenga vituo kadhaa vinavyotumiwa na wanamgambo wa Hezbollah kusini mwa Beirut kupanga operesheni zao.

Shirika la habari la Lebanon NNA limeripoti kuwa shambulio la droni la Israel lilipiga jumba moja katika eneo la Beddawi karibu na Tripoli, na kumuua afisa mwandamizi wa Hamas, Wassim Atallah al-Ali, pamoja na mke wake.

 

Kiongozi wa Hezbollah, Naim Qassem, ameapa kuendeleza mapambano dhidi ya Israel, akisema kundi lake limefanya takriban mashambulizi 15 yaliyolenga maeneo ya Israel, ikiwemo Tel Aviv.

Katika hotuba yake ya kwanza tangu mashambulizi ya pamoja ya Marekani na Israel dhidi ya Iran kuanza, Qassem amesema kamwe hawatarudi nyuma na wako tayari kupigana "hadi dakika ya mwisho."

Mamlaka za Lebanon zimeripoti kuwa watu 72 wameuawa, 437 wamejeruhiwa na zaidi ya 83,000 wameyahama makazi yao tangu Jumatatu.

Iran imelipiza kisasi kwa kushambulia maeneo yanayohusishwa na Marekani katika mataifa ya Ghuba pamoja na miundombinu ya nishati. Milipuko imesikika mapema leo katika miji mikuu ya Doha, Qatar na Manama nchini Bahrain.

Safari za ndege zavurugika Mashariki ya Kati

02:00

This browser does not support the video element.

Tangu vita hivyo kuanza, watu 13 wameuawa katika mataifa ya Ghuba—wakiwemo raia saba—akiwemo pia msichana wa umri wa miaka 11 nchini Kuwait.

Qatar imesema imewahamisha watu wanaoishi karibu na ubalozi wa Marekani mjini Doha, baada ya kudai kuwa ilizuia mashambulizi yaliyolenga Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Hamad.

Mataifa ya Umoja wa Falme za Kiarabu, Saudi Arabia na Qatar yameripoti kuzuia makombora ya Iran, ikiwemo droni iliyokuwa ikilenga kiwanda kikubwa cha kusafisha mafuta cha Ras Tanura nchini Saudi Arabia.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW