1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mashambulizi mapya Syria.

28 Oktoba 2016

Waasi nchini Syria, ikiwa ni pamoja na wapiganaji wa jihad leo hii wameanzisha mashambulizi ya kushtukiza dhidi ya majeshi ya serikali na washirika wake yanayolenga kuvunja mzingiro wa majeshi ya serikali.

Syrien Aleppo Offensive der Rebellen
Picha: picture-alliance/abacaB. El Halebi

Mashambulizi hayo, yaliyohusisha mashambulizi ya mabomu na magari yaliyotumiwa na waasi hao kujitoa muhanga yalilenga zaidi katika eneo la pembe ya Magharibi mwa mji huo wa Aleppo, yanayokaliwa na waasi na ambayo yako nje ya mji. Miongoni mwa maeneo hayo, ni Jabhat Fateh al-Sham, ambalo awali lilitumiwa na kundi la Nusra Front, lilikuwa na mahusiano na kundi la kigaidi la al-Qaeda na makundi yanayopambana chini ya bendera ya vikosi huru vya Syria. 

Shirika la Haki za Binaadamu la Syria lenye makao yake nchini Uingereza limesema zaidi wa raia 15 wameuwawa na wengine 100 wakijeruhiwa kutokana na mashambulizi hayo ya waasi dhidi ya maeneo yanayozingirwa na serikali katika eneo hilo la mashariki mwa Aleppo. Hata hivyo, shirika la habari la serikali limesema ni watu watano tu wameuwawa.

Picha zinaonyesha waasi hao wakikaribia Aleppo wakiwa na vifaru, magari yaliyosheheni silaha, buldoza, magari ya wazi na pikipiki, lakini pia moshi mkubwa unaofuka baada ya milipuko ya mabomu.

Waasi wanasema, wamekwishachukua baadhi ya maeneo kutoka kwa majeshi ya serikali. Hata hivyo chanzo cha habari kutoka jeshi la Syria kinasema shambulizi katika eneo hilo la Magharibi ya mji lilizimwa. Kituo cha televisheni cha serikali kimetangaza kuwa jeshi hilo limeshambuli na kuharibu magari manne ya waasi yaliyokuwa na mabomu.

Picha ikionesha mmoja wa watoto wanaokosa masomo kutokana na mashambulizi ya shule, Aleppo.Picha: picture-alliance/AA/R. Maltas

Awali, Umoja wa mataifa na baadhi ya nchi wanachama zimetoa mwito wa uwajibikaji kufuatia shambulizi la anga kwenye shule katika eneo linaloshikiliwa na serikali, Magharibi mwa Aleppo hapo jana na kusababisha vifo vya watoto na walimu, ikiwa ni siku moja tu baada ya shambulizi jingine kwenye shule iliyoko kijiji cha Idlib, kilichopo kwenye eneo linaloshikiliwa na waasi. 

Mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa kwenye masuala ya elimu na waziri mkuu wa zamani wa Uingereza, Gordon Brown ameliita kwa uwazi shambulizi hilo kuwa ni uhalifu wa kivita.

Katibu Mkuu wa umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon nae amelaani vikali shambulizi hilo lilisababisha vifo vya raia 35, ambao ni pamoja na wanafunzi 22 na walimu 6, huku akitaka kufanyike kwa uchunguzi wa haraka, amesema Stephane Dujarric, ambaye ni msemaji wa Ban. Hata hivyo, Urusi inayolaumiwa na mashambulizi hayo imekanusha kuhusika.

Balozi wa Uingereza kwenye Umoja wa Mataifa, Matthew Rycroft ,amekubaliana na mwito wa uwajibikaji, ingawa ameonyesha wasiwasi wake iwapo Baraza la Usalama la Umoja huo litaweza kuliwasilisha tukio hilo kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, ICC, kwa kuzingatia kwamba Urusi inayounga mkono serikali la Syria, analindwa na kura ya VETO, na hata awali hakufikishwa kwenye mahakama ya Umoja wa mataifa dhidi ya tuhuma za kumuunga mkono Bashar al-Assad.

Mwandishi: Lilian Mtono/Reuters/AP/dpa
Mhariri: Mohammed Khelef

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW