1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mashambulizi mengine ya kielektroniki yaitikisa Lebanon

Angela Mdungu
19 Septemba 2024

Awamu mpya ya mashambulizi ya kielektroniki imeitikisa tena Lebanon na imesababisha vifo vya watu wasiopungua 20. Kulingana na shirika la habari la nchi hiyo watu wengine 450 wamejeruhiwa.

Vifaa vya mawasiliano vimelipuka na kuwauwa watu 20 Lebanon
Magari ya kubeba wagonjwa yakiwasili kutoa huduma kwa waathiriwa wa mlipuko wa vifaa vya mawasiliano nchini LebanonPicha: FADEL ITANI/AFP

Vifaa vya mawasiliano vikiwemo, simu za upepo zinazofahamika pia kama radio call na taa zinazotumia jua kuzalisha umeme, vililipuka Jumatano ikiwa ni saa kadhaa baada ya shambulio la awali lililovilenga vifaa vya mawasiliano vinavyotumiwa na wanamgambo wa Hezbollah nchini Lebanon. Shambulio la awali lilisababisha vifo vya watu tisa na takriban watu 2800 walijeruhiwa.

Mashambulizi hayo yanayodaiwa kufanywa na Israel yakiwalenga wanamgambo hao, yamesababisha pia mauaji ya raia na kuibua hofu kuwa, mzozo wa pande hizo mbili huenda ukatanuka zaidi.

Soma zaidi: Hezbollah yailaumu Israel kwa mashambulizi ya kieletroniki Lebanon

Waziri wa Afya wa Lebanon Firass Abiad ameyalaani mashambulizi hayo akisema kuwa  "Kitendo hiki ni cha kuwashambulia raia wa kawaida. Hata kama mtu au miongoni mwao ni wapiganaji, mashambulizi haya hayabagui. Nafikiri matumizi ya vifaa visivyobagua kufanya mashambulizi, ambavyo ni wazi vinaweza kuwaathiri raia ni jambo ambalo ni kinyume cha sheria ya kimataifa"

Kampuni ya Japan inayohusishwa na utengenezaji wa toleo la sehemu ya vifaa vilivyolipuliwa  imekanusha kuwa ilihusika kutengeneza vifaa hivyo.

Mashambulizi hayo yanajiri baada ya Waziri wa Ulinzi wa Israel kusema Jumatano mbele ya wanajeshi wake kuwa, nchi yake iko katika awamu mpya ya vita inayohitaji ujasiri, dhamira ya dhati na ustahimilivu.

Simu ya upepoPicha: Anwar Amro/AFP

Ujerumani yataka pande hasimu zijizuie Mashariki ya Kati

Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Ujerumani Anarlena Baerbock amezitaka pande zinazohusika na mzozo wa Mashariki ya Kati kujizuwia baada ya shambulio hilo huku Uturuki ikiituhumu Israel kwa kutaka kuvitanua vita vya Gaza hadi Lebanon.

Hayo yakiendelea, jeshi la Israel limesema Alhamisi kuwa, jeshi lake la anga limeishambulia miundombinu kadhaa ya wanamgambo wa Hezbollah Kusini mwa Lebanon. Miongoni mwa miundombinu hiyo ni ghala la kuhifadhi silaha katika eneo la Khiam.

Soma zaidi: Hezbollah yaapa kulipa kisasi mashambulizi dhidi ya Lebanon

Katika hatua nyngine vikosi vya usalama vya Israel vimesema kuwa vimemkamata raia nchi hiyo anayetuhumiwa kutumiwa na Iran katika njama za kutaka kumuuwa Waziri Mkuu, Benjamin Netanyahu. Kulingana na taarifa ya polisi na shirika la ndani la ujasusi la Israel Shin Bet mtu huyo alifundishwa na Iran kuhamasisha mauaji ya viongozi kadhaa wa Israel. Taarifa hiyo inasema raia huyo wa Israel ameshawahi kuingia Iran mara mbili na kupokea malipo ili kukamilisha mpango huo.

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW