1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIran

Mashambulizi mapya yatikisa Ghuba ya Uajemi

3 Juni 2026

Marekani na Iran zimeendeleza mashambulizi katika Ghuba ya Uajemi na kuzidisha mvutano katika eneo hilo. Mapigano hayo yanatokea wakati juhudi za amani zikiwa bado zimekwama bila mafanikio makubwa.

Lebanon |
Mashambulizi mapya yanaweka katika mtihani makubaliano ya kusitisha mapigano.Picha: Kawant Haju/AFP

Nchini Kuwait, uwanja wa ndege wa kimataifa ulilengwa katika shambulio lililosababisha uharibifu mkubwa na kujeruhi watu kadhaa. Kufuatia tukio hilo, mamlaka za usafiri wa anga zilisitisha safari zote za ndege na kuelekeza ndege zinazoingia katika viwanja vingine vya ndege. Shirika la ndege la Kuwait Airways pia limesimamisha shughuli zake kwa muda.

Wakati huo huo, Bahrain imesema ilifanikiwa kudungua makombora matatu na ndege kadhaa zisizo na rubani zilizokuwa zikielekezwa nchini humo. Jeshi la Marekani kupitia Kamandi Kuu ya Operesheni zake, CENTCOM, limesema makombora mengine ya Iran yalishindwa kufikia shabaha yake au yaliharibika yakiwa angani.

Marekani pia imetangaza kuwa imedungua ndege zisizo na rubani za Iran zilizokuwa zikilenga meli za kiraia na vikosi vya Marekani katika eneo la Ghuba, na kufanya mashambulizi katika Kisiwa cha Qeshm karibu na Mlango wa Hormuz. Iran, kupitia Kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu, IRGC, imedai kushambulia makao makuu ya Jeshi la Wanamaji la Marekani la Fifth Fleet nchini Bahrain pamoja na vituo vingine vya kijeshi katika eneo hilo.

Mashambulizi haya yanaweka katika mtihani makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyofikiwa mwezi Aprili, ambayo yamekuwa yakivunjwa mara kwa mara tangu vita vilivyochochewa na mashambulizi ya Marekani na Israel dhidi ya Iran.

Mkwamo katika mazungumzo ya amani

Katika matukio mengine, mapigano kati ya Israel na Hezbollah yameendelea kusini mwa Lebanon huku maafisa wa Lebanon na Israel wakifanya mazungumzo ya moja kwa moja mjini Washington.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubia ameliambia Bunge la Marekani kuwa hakutakuwa na unafuu wa vikwazo dhidi ya Iran. Picha: Arun Sankar/AFP

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, amesema Hezbollah ndiyo kikwazo kikuu kinachozuia kufikiwa kwa makubaliano ya amani kati ya pande hizo mbili.

Rubio pia ameliambia Bunge la Marekani kuwa hakutakuwa na unafuu wa vikwazo kwa Iran ili kufungua tena Mlango wa Hormuz, akieleza kwamba hatua yoyote ya kuondoa vikwazo itategemea Iran kuachana kabisa na shughuli zake za nyuklia.

"Iran inawekewa vikwazo kwa sababu wanarutubisha urani. Inawekewa vikwazo kwa sababu wana urani iliyorutubishwa kwa kiwango cha juu. Inawekewa vikwazo kutokana na shughuli zake za nyuklia. Ikiwa watakubali kuachana na mambo hayo, kutakuwa na unafuu wa vikwazo kulingana na ahadi na utekelezaji wao.”

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amewasilisha mapendekezo matatu kwa Baraza la Usalama yenye lengo la kuimarisha usimamizi wa mpaka wa Israel na Lebanon, kusaidia jeshi la Lebanon kuimarisha uwepo wake nchini kote, na kuimarisha juhudi za kisiasa za kumaliza mapigano.

Guterres amesema utekelezaji wa azimio la mwaka 2006, lililomaliza vita kati ya Israel na Hezbollah, ni muhimu kwa amani.  Azimio hilo linataka Hezbollah iweke silaha kando, Israel iondoe majeshi yake, na jeshi la Lebanon liwe jeshi pekee nchini, lakini hatua hizo bado hazijatekelezwa.

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW