1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yaanzisha mashambulizi mapya Gaza

Angela Mdungu
24 Julai 2024

Majeshi ya Israel yamefanya mashambulizi mapya katika Ukanda wa Gaza Jumatano, saa kadhaa kabla ya Waziri wake Mkuu Benjamin Netanyahu kulihutubia Bunge nchini Marekani

Khan Younis, Ukanda wa Gaza
Moshi ukifuka baada ya mashambulizi ya Israel katika mji wa Khan Younis 22/07/2024Picha: Abdel Kareem Hana/AP Photo/picture alliance

Mashambulizi  mapya yaliyoanzishwa na Israel yameyaangamiza makazi ya miji iliyo mashariki mwa Khan Younis, kusini mwa Gaza. Wakaazi wanasema, maelfu ya watu wamelazimika kukimbilia magharibi mwa eneo hilo ili kutafuta mahali pa kujisitiri.

Jeshi hilo limefanya pia mashambulizi ya anga katika maeneo kadhaa katikati na Kaskazini mwa Gaza ikiwemo katika kambi ya wakimbizi ya Al-Bureij. Maafisa wa wizara ya afya chini ya kundi la Hamas wanasema watu tisa wameuwawa katika shambulio la Al Bureij.

Kulingana na Jeshi hilo la Israel limekuwa likifanya operesheni zake kwenye maeneo ambayo wapiganai wa Palestina wamekuwa wakiyatumia kurusha roketi ndani ya Israeli na kuwashambulia wanajeshi wake.

Duru za habari zimeripoti pia afisa mmoja wa Polisi wa maadili katika Mamlaka ya Palestina, aliuwawa Jumanne usiku katika kijiji cha Tubas wakati Israel ilipofanya operesheni ya kijeshi katika Ukingo wa Magharibi.

Soma zaidi: Wizara ya afya ya Gaza yasema watu 39,145 wameuwawa katika vita

Hayo yakijiri, hali ya kiutu na huduma za afya katika ukanda huo zimeendelea kuzorota.  Shirika la Afya duniani WHO limesema  takriban watu 14,000 wanahitaji kupelekwa nje ya ukanda huo kwa ajili ya matibabu.

Wapalestina waikosoa Marekani kwa kumpokea Netanyahu

Wakati huohuo, baadhi ya Wapalestina waliokusanyika katika Hospitali ya Khan Younis kabla ya maziko ya jamaa zao waliouwawa kwa mashambulizi ya Israel, wameikosoa Marekani kwa kumkaribisha Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu.

Rais wa Marekani Joe Biden na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin NetanyahuPicha: Brendan Smialowski/AFP

Kwa upande wake Afisa wa ngazi ya juu wa kundi la Hamas, Sami Abu Zuhri ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa mwaliko wa bunge la Marekani kwa Netanyahu, na kumpa nafasi ya kuhutubia unampa uhalali wa uhalifu, vita na mauaji yanayoendelea Gaza. Amesema, kumpokea Netanyahu ni aibu kwa Wamarekani wote.

Netanyahu atalihutubia bunge la Marekani akikabiliwa pia na ukosoaji mkubwa kutoka kwa Rais wa Marekani Joe Biden na baadhi ya wanachama wa ngazi za juu wa chama cha Biden juu ya namna anavyoendesha vita katika ukanda wa Gaza.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW