1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mashambulizi mapya zaidi Syria

Admin.WagnerD14 Oktoba 2016

Ndege za kivita za Syria na Urusi zimeendelea kufanya mashambulizi katika ngome za waasi mjini Aleppo na kuua watu 150

Syrien Aleppo Bergung Opfer Luftangriff
Picha: picture-alliance/AA/I. Ebu Leys

Mashambulizi mapya zaidi yameendelea kufanywa katika mji wa Aleppo hasa maeneo yanayodhibitiwa na waasi. Hayo yanajiri wakati rais wa syria Bashar al-Assad akisema kuwa ikiwa jeshi la serikali yake litafaulu kudhibiti mji wa Aleppo basi itakuwa hatua muhimu katika kile alichokiita ''kuwalazimisha magaidi hao kurejea Uturuki''.

Ndege za kivita za Syria na Urusi zimeendelea kufanya mashambulizi katika ngome za waasi mjini Aleppo. Kulingana na mkuu wa kundi linalochunguza haki za binadamu nchini Syria Rami Abdel Rahman, mashambulizi hayo yameshuhudiwa katika saa kadhaa tangu alfajiri ya Ijumaa. Hata hivyo idadi ya waliouawa au kujeruhiwa bado haijajulikana.

Msemaji wa kundi la wasamaria wema la White Helmets ambalo pia hutoa huduma za misaada Aleppo Ibrahim Abu al-Leith, amesema bado kuna watu wamekwama ndani ya majengo yaliyoporomoshwa kutokana na mashambulizi hayo, na waokoaji wangali wanajaribu kuwanusuru.

Rais wa syria Bashar al-Assad kwa upande wake amesisitiza haja ya kuwaondoa waasi katika eneo hilo au kuwaua. "Huwezi ukasitisha, lazima usafishe. Lazima uendelee kusafisha eneo hili na uwasukume magaidi kurudi Uturuki mahali walitoka ama uwaue. Hakuna mbinu nyingine. Lakini kudhibiti mji wa Aleppo kutakuwa hatua muafaka kufanikisha hilo na kukomboa ngome nyinginezo"

Awali jeshi la Syria lilitangaza kuwa lingalipunguza mashambulizi ili kuruhusu raia wajiondoe katika ngome za waasi. Lakini wiki hii, mashambulizi yalianza upya. Tangu tarehe 22 Septemba ambapo Syria ilitangaza mashambulizi makali yenye lengo la kuudhibiti mji wa Aleppo, inakadiriwa kuwa zaidi ya watu 370 wakiwemo watoto 70 wameuawa kufuatia mashambulizi hayo yanayofanywa na Syria kwa ushirikiano na Urusi.

Picha: Picture-Alliance/Epa/Sana

 Mapema wiki hii, katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon aliyasihi makundi yanayopigana  Aleppo kusitisha vita mara moja ili kuruhusu shughuli za kuwaondoa raia na watoto kufanywa.

Inakadiriwa kuwa watu 250,000 wangali wanaishi mashariki ya Aleppo, eneo ambalo limekuwa ngome ya waasi tangu mwaka 2012.

Siku ya Alhamisi wiki hii, Urusi ilisema ipo tayari kuwapa ulinzi waasi ambao watataka kuondoka Aleppo. Urusi imekumbwa na lawama tele za kimataifa kuhusu mauaji ya raia mjini Aleppo kutokana na mashambulizi yake.

Tangu kuvunjika kwa mkataba wa usitishwaji vita kati ya Urusi na Marekani mwezi jana, maeneo ya Aleppo yamekumbwa na mapigano makali kuwahi shuhudiwa kwa kipindi cha miaka mitano ya vita hivyo.

Waziri wa mambo ya nje nchini Marekani John Kerry na mwenzake wa Urusi Sergei Lavrov wanatarajiwa kukutana siku ya Jumamosi-kesho mjini Lausanne-Uswisi, kuanza upya mazungumzo ya usitishwaji vita Syria. Washirika wengine wanaotarajiwa kwenye mazungumzo hayo ni Uturuki, Saudi Arabia na Qatar ambao wote wanaunga mkono waasi wanaopinga serikali ya Syria.

Lakini maafisa wa Marekani wameliambia shirika la habari la reuters kuwa rais Barrack Obama na wakuu wa ushauri wa sera, wanatarajiwa kukutana leo, kujadili uwezekano wa kutumia mbinu ya kijeshi na nyinginezo katika machafuko ya Syria. Maafisa wengine wamesema Marekani sasa haina budi kutumia nguvu kuhusu Syria au itapoteza ushawishi wake. Hata hivyo wanatilia shaka ikiwa Obama ataidhinisha matumizi ya nguvu za kijeshi.

     

Mwandishi: John Juma/AFPE/RTRE/APE

Mhariri: Gakuba Daniel