Mashambulizi ya anga yaua watu 10 Somalia
21 Desemba 2011Mkazi mmoja wa kijiji hicho Mohammed Gelle aliliambia shirika la habari la Reuters kuwa maduka katika sehemu hiyo yalikuwa yakiwaka moto. Kijiji cha Hosungow kiko katika eneo la Dhobley karibu na mpaka kati ya Somalia na Kenya.
Haikujulikana mara moja ndege hizo zilitumwa na upande gani, lakini jeshi la Kenya ambalo mwezi Oktoba lilivuka mpaka na kuingia Somalia kuwasaka wanamgambo wa Al Shababu, limekuwa likizidisha mashambulizi ya anga katika wiki za hivi karibuni. Wakazi wa kijiji cha Hosungow walisema wengi wa waliokufa ni raia, na waliojeruhiwa walipelekwa majumbani mwao kwa sababu eneo hilo halina kituo cha afya.
Msemaji wa serikali ya Somalia Mahmoud Farah aliiambia Reuters kwamba kilicholengwa na ndege hizo kilikuwa kituo kinachotumiwa na Al Shababu kutoa mafunzo kwa wapiganaji wake, na kuongeza kuwa hasara kwa wanamgambo hao kutokana na mashambulizi ya jana ilikuwa kubwa.
Ingawa Al Shababu imekiri kuwa mashambulizi hayo yalifanywa, msemaji wake Abdiasis Abu Musab alisema hakuna hasara yoyote iliyotokea kwa upande wao.
Wakati hayo yakiarifiwa, ndege iliyobeba kikosi cha kwanza cha wanajeshi wa Djibouti wanaokwenda kujiunga na mapambano dhidi ya Al Shababu ilitua jana mjini Mogadishu. Ripoti iliyotolewa kufuatia kuwasili kwao, ilisema kikosi hiki cha kwanza kinawajumuisha wanajeshi 100, na kuongeza kuwa wengine wapatao 800 watafuatia katika kipindi cha wiki moja.
Naibu Kamanda wa vikosi vya Umoja wa Afrika vya kulinda amani nchini Somalia, AMISOM, Brigadia Jenerali Audace Nduwumunsi alisema kikosi cha Djibouti kitaweka kambi katika eneo la Al Jazeera IV kusini mwa mji mkuu Mogadishu. Alisema kuwasili kwa kikosi hicho ni hatua muhimu kuimarisha AMISOM na juhudi zake kuleta utulivu nchini Somalia. Kenya pia inataka jeshi lake liingizwe katika mpango wa kulinda amani nchini Somalia chini ya uongozi wa AMISOM.
Wanamgambo wa Al Shababu wenye mafungamano na kundi la kigaidi la al Qaida wanashikilia sehemu kubwa kusini mwa Somalia, lakini shinikizo limekuwa likipamba moto dhidi yao siku za hivi karibuni, na wamelazimika kuzihama ngome zao mjini Mogadishu na kugeukia mbinu ya vita vya msituni.
Mwandishi: Daniel Gakuba/AFPE
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman