Mashambulizi ya angani yaanza tena Yemen
18 Mei 2015Hatua hii imetokea baada ya kumalizika hapo jana usiku kwa muda wa usitishaji mapigano uliolenga kutoa nafasi ya kufikisha misaada ya kwa waathirika wa mgogoro huo.
Akizungumza na shirika la habari la Reuters, Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Yemen amesema muungano unaoongozwa na Saudi Arabia umeamua kutoendeleza kipindi cha kusitisha mapigano kwa sababu makubaliano ya awali yalikiukwa mara kadhaa na waasi wa Houthi.
"Hicho ndicho tulichokisema awali – kwamba wakianza tena tutaanza tena," alisema Reyad Yassin Abdullah anayetokea upande wa serikali ya Yemen iliyoko uhamishoni mjini Riyadh nchini Saudi Arabia. Ameongeza kuwa muungano huo hautarajii kuwa na makubaliano yoyote mapya ya kusitisha mapigano.
Hata hivyo waasi wa Houthi hawakupatikana mara moja kutoa maoni yao juu ya hilo.
Mabomu ya angani yalidondoshwa katika ikulu ya rais inayoshikiliwa na waasi mjini Aden, na dhidi ya makundi ya wanamgambo Magharibi na Mashariki mwa mji huo na pia kwenye uwanja wa ndege wa Kimataifa ambako waasi wa Kihouthi na wapiganaji wamekuwa wakipambana. Hii ni kulingana na wakaazi wa maeneo hayo. Bado hapajakuwa na habari zaidi juu ya majeruhi wa mkasa huo.
Kwa zaidi ya wiki sita, Saudi Arabia na washirika wake wa Kisunni wamekuwa wakiwashambulia waasi wa jamii ya Houthi na vikosi vya wanajeshi watiifu kwa rais wa zamani wa Yemen Ali Abdullah Saleh. Muungano huo unasema waasi hao wanaungwa mkono na taifa la Waislamu wa Kishia la Iran.
Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Iran azungumzia hali ilivyo Yemen
Wakati huo huo waziri wa mambo ya nchi za nje wa Iran Mohammed Javad Zariff ameutaka Umoja wa Mataifa kuchukua jukumu zaidi nchini Yemen ikiwemo kuingia ndani ya Yemen kuhakikisha misaada ya kiutu inasambazwa.
"Bila shaka Umoja wa Mataifa unaweza kuchunguza na kuhakikisha misaada inayopelekwa kwa watu wa yemen, ni misaada ya kiutu, ni muhimu pia kupeleka msaada wa matibabu kwa wagonjwa na waliojeruhiwa, kwahivyo tunazihitaji jitihada za jamii ya kimataifa ili kuishughulikia Yemen," alisema waziri Zariff.
Makubaliano ya siku tano ya kusitisha mapigano yalioanza usiku wa Jumanne yalisimamisha mashambulizi ya angani na kutoa nafasi ya misaada ya kiutu katika nchi hiyo iliozingirwa, lakini wakaazi wa maeneo ya kusini mwa Yemen kama Shabwa, Dhalea na Abyan wamesema mapigano makali ya ardhini yaliendelea licha ya makubaliano hayo.
Kwa upande wake Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani John Kerry amesema nchi yake inaunga mkono hatua ya kuendeleza makubaliano ya kusitisha mapigano lakini ujanja unaofanywa na waasi wa Houthi unaifanya hatua hiyo kuwa ngumu kutekelezwa. Aidha mjumbe mpya wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia mzozo wa Yemen Isamil Ould Cheikh Ahmed ametoa wito wa makubaliano ya kusitisha mapigano kurefushwa.
Mwandishi Amina Abubakar/Reuters
Mhariri: Iddi Ssessanga