1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Boko Haram yawaua zaidi ya watu 30 Nigeria

23 Julai 2015

Kiasi ya watu 37 wameuawa na wengine zaidi ya mia moja wamejeruhiwa katika miripuko iliyovilenga vituo vya mabasi na soko katika mji wa kaskazini Mashariki ya Nigeria wa Gombe.

Picha: picture-alliance/dpa

Afisa wa shirika la msalaba mwekundu nchini Nigeria Abubakar Yakubu amesema mashambulizi hayo ya mabomu yaliyotokea hapo jana jioni yamesababisha vifo vya zaidi ya watu 30 na wengine 105 wamejeruhiwa na kupelekwa katika hospitali ya Gombe kwa matibabu.

Walioshuhudia mashambulizi hayo wamesema idadi ya wathiriwa inatarajiwa kuongezeka. Mashambulizi hayo ya jana jioni ni ya hivi karibuni katika msururu wa mashambulizi kaskazini mwa Nigeria yanayoshukiwa kufanywa na waasi wa Boko Haram ambayo yamesababisha vifo vya zaidi ya watu 430 mwezi huu peke yake.

Bomu la kwanza liliripuliwa mwendo wa saa moja usiku na mshambuliaji wa kujitoa muhanga katika msikiti wa Dadin wakati waumini walipokuwa wamekusanyika kusali.

Mji wa Gombe washambuliwa tena

Shambulizi jingine lilitokea katika kituo kikubwa cha mabasi cha Duku na katika soko liloko karibu na kituo hicho. Shirika la kitaifa la kushughulikia mikasa ya dharura limetoa wito kwa watu kujitokeza kutoa damu ili kuwasaidia waliojeruhiwa kutibiwa. Kiasi ya watu 50 waliuawa katika mji huo huo wa Gombe Ijumaa iliyopita na waasi wa Boko Haram.

Waliojeruhiwa katika shambulizi la GombePicha: picture-alliance/dpa

Na katika nchi jirani ya Cameroon maafisa wamesema leo Boko Haram imefanya pia mashambulizi na kuwaua watu 24 na kuwajeruhi wengine 50 katika soko moja lililoko mpakani kati ya Cameroon na Nigeria.

Hayo yanakuja baada ya Rais wa Nigeria Muhammadu Buhari kuonya kuwa kukataa kwa Marekani kuiuzia nchi yake silaha muhimu na za kisasa kunawasaidia waasi wa Boko Haram kuendeleza uasi nchini Nigeria.

Buhari aitaka Marekani kuipa Nigeria silaha

Rais Buhari amerejea leo nchini Mwake kutoka Marekani ambako amefanya ziara ya siku nne ambako alipokelewa vyema na Rais Barack Obama lakini alishindwa kupata kile alichotarajia kutoka kwa Marekani, kubwa miongoni mwao kikiwa kuuziwa silaha za kupambana na Boko Haram.

Rais wa Nigeria Muhammadu Buhari na Rais wa Marekani Barack ObamaPicha: Reuters/K. Lamarque

Buhari amewaambia watunga sera katika taasisi ya Marekani kuhusu amani kuwa jeshi la Nigeria limeshindwa kwa kiasi kikubwa kutokana na kutokuwa na silaha za kisasa za kupambana na waasi wa Boko Haram na kumhimiza Rais Obama, bunge la Marekani na serikali kutafuta njia za kulegeza sheria inayopiga marufuku uuzaji wa silaha fulani kwa nchi ambayo jeshi lake linatuhumiwa kwa ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu.

Shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu la Amnesty International linalituhumu jeshi la Nigeria kwa kuwaua watu 8,000 waliokuwa kizuizini, idadi mara ya mbili ya watu waliouawa na Boko Haram katika kipindi cha miaka minne ya kwanza ya uasi wa kundi hilo ambao umedumu kwa miaka sita sasa.

Mwandishi:Caro Robi/Reuters/ap

Mhariri: Daniel Gakuba