1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mashambulizi ya Israel kuidhoofisha Hamas

14 Julai 2014

Israel inataraji kusababisha uharibifu mkubwa kwa miundo mbinu ya kundi la Hamas kabla ya kukubali kuwa na mzungumzo ya kusitisha mapigano wakati mashambulizi ya Israel yakiingia siku ya saba Jumatatu (14.07.2014) Gaza.

Moshi ukifuka kufuatia mashambulizi ya Israel katika Ukanda wa Gaza.
Moshi ukifuka kufuatia mashambulizi ya Israel katika Ukanda wa Gaza.Picha: picture-alliance/dpa

Israel inaonekana haina haraka ya kuanzisha operesheni ya ardhini dhidi ya Ukanda wa Gaza iliokuwa imetishia,wakati ndege zake zikiendelea kushambulia Gaza na kufanya idadi ya Wapalestina waliouwawa hadi sasa kufikikia 172 huku wanamgambo wakiendelea kuvurumisha maroketi katika eneo la kati la Israel na kusababisha maelfu kukimbia kutafuta hifadhi katika miji mikubwa ya Israel.

Waziri wa Fedha wa Israel Yair Lapid ameiambia radio ya jeshi hapo jana kwamba kwa sasa serikali ya Israel haishughuliki na juhudi za kusitisha mapigano kwa sababu kwanza wanataka kujuwa kwamba wameweza kutokomeza shauku ya Hamas kuvurumishia tena makombora Israel kwa mwaka mwengine mmoja au miezi sita.Amesema hilo halikufanyika bado na kwamba watazungumza baada ya hilo kufanyika.

Hadi sasa mashambulizi ya kijeshi ya Israel yamekuwa kwa kiasi kikubwa ni ya anga tu.Mkuu wa zamani wa ujasusi wa kijeshi wa Israel Amos Yadin amesema jeshi la Israel IDF limeishambulia vibaya Gaza lakini haikushambulia vya kutosha kitengo cha kijeshi cha Hamas na kwamba hadi sasa ni asilimia hamsini tu ya wahanga wa mashambulizi hayo inaaminika kuwa ndio wanachama wa kundi hilo.

Kudhoofisha Hamas

Amesema wanajaribu kukidhoofisha kitengo cha kijeshi cha Hamas na kuimarisha msimamo wa Israel katika mazungumzo ya kusitisha mapigano pamoja na kuathiri uwezo wa Hamas wa kuwa na nguvu baada ya operesheni hiyo.

Wanajeshi wa Israel kwenye mpaka wa Gaza na Israel.Picha: picture-alliance/dpa

Juu ya kwamba Israel imekusanya vifaru na vikosi kwenye mpaka wake na Gaza jambo linalothibitisha kwamba iko tayari kwa shambulio la ardhini mawaziri katika mkutano uliodumu hadi wa usiku wa manane hapo jana umeamuwa kutotuma wanajeshi wake kwa sasa kwa ajili ya operesheni hiyo.

Licha ya shinikizo hilo Hamas pia haikuonyesha hamu ya kutaka suluhu ikisisitiza Israel ikomeshe uchokozi dhidi ya Gaza,kuacha vikwazo iliyoiwekea kwa miaka minane sasa na kuwaachia huru mamia ya watu wake wanaotiwa magerezani kutokana na msako unaoendelea hivi sasa huko Ukingo wa Magharibi.

Maelfu watafuta hifadhi

Maelfu ya Wapalestina wamekuwa wakiyakimbia mashambulizi hayo ya Israel katika Ukanda wa Gaza na wengine wamekuwa wakijihifadhi katika shule zinazosimamiwa na Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia wakimbizi wa Kipalestina UNRWA huko Gaza.

Wapalestina wakikimbia mashambulizi ya Israel katika Ukanda wa Gaza.Picha: Reuters

Manar al Attar mmojawapo wa wakimbizi hao amesema

"Hatukuja hapa kunusuru roho zetu bali zile za watoto wetu wanaomka saa saba za usiku wakiwa na hofu. Tumeziacha nyumba zetu na vitu vyetu, tumeacha kila kitu na kuja hapa ambapo hakuna chochote na tunaishia katika maisha yalio chini ya kiwango cha wanyama."

Mawaziir wa mambo ya nje wa Jumuiya ya Waarabu watakutana Cairo baadae leo hii kujadili mashambulizi hayo ya Israel dhidi ya Gaza yenye lengo la kukomesha kuvurumishwa kwa maroketi nchini Israel kunakofanywa na wanamgambo wa Kipalestina.

Kumekuwepo na maandamano katika miji mbali mbali mikubwa barani Ulaya, Marekani na hadi Asia kulaani mashambulizi hayo ya Israel.

Mwandishi : Mohamed Dahman/AFP

Mhariri : Mohammed Abdul-Rahman

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW