1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mashambulizi ya Israel Gaza yaua 15 katika shule ya UN

Angela Mdungu
4 Novemba 2023

Wizara ya afya ya Gaza imesema watu wasiopungua 15 wameuwawa leo baada ya Israel kuishambulia shule ya Umoja wa Mataifa ya Al Fakhura iliyokuwa ikiwahifadhi raia waliolazimika kuyahama makazi yao.

Wakazi wa Gaza wakiangalia uharibifu baada ya mashambulizi ya Israel huko Gaza
Wakazi wa Gaza wakiangalia uharibifu baada ya mashambulizi ya Israel huko GazaPicha: Bashar Thaleb/AFP

Vile vile, msemaji wa wizara hiyo ameeleza kuwa watu 70 wamejeruhiwa kutokana na mashambulizi hayo. Kulingana na wizara hiyo, hadi sasa zaidi ya watu 9,400 wameshapoteza maisha tangu vita vya Israel dhidi ya kundi la Hamas vilipoanza baada ya kundi hilo kufanya shambulio lililowauwa Waisrael 1,400 Oktoba saba.

Nalo Jeshi la Israel, kwa mara nyingine limewapa wakaazi wa Ukanda wa Gaza muda wa saa tatu kukimbilia upande wa kusini mwa ukanda huo. Msemaji wa jeshi hilo kupitia ukurasa wake wa mtandao wa X kwa kutumia lugha ya kiarabu alitoa tangazo hilo saa moja kabla ya kuanza kwa muda waliotakiwa kuondoka wakaazi hao. Pamoja na amri hiyo, jeshi la Israel limechapisha ramani inayoonesha njia wanazopaswa kutumia raia hao wa Palestina.

Soma zaidi: Netanyahu akataa miito ya kusitishwa vita Gaza

Hayo yanajiri wakati Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani, Antony Blinken akikutana na viongozi wa mataifa ya Kiarabu katika juhudi za kusitisha mapigano huko Gaza.

Tukisalia katika mzozo huo, kundi la Hezbollah la Lebanon limesema limefanya mashambulizi kadhaa kwa mpigo dhidi ya Israel katika mpaka wa nchi hizo. Chanzo chenye ufahamu kuhusu mashambulizi ya Hezbollah kimesema kundi hilo lilirusha makombora ya nguvu ambayo hayajawahi kutumika kutoka katika vijiji vya  Ayta al-Shaab na Rmeich.

Soma zaidi: UN yahitaji dola bilioni 1.2 kuwasaidia Wapalestina

Nalo jeshi la Israel limesema katika kujibu mashambulizi hayo ndege zake za kivita zilishambulia miundombinu ya Hezbollah. Jeshi hilo limesema lilifanya pia mashambulizi dhidi ya kundi hilo kwa kutumia makombora na vifaru.

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW