1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mashambulizi ya Israel yaua 42 ndani ya saa 24 huko Gaza.

2 Novemba 2024

Msururu wa mashambulizi ya Israel katika kambi ya wakimbizi ya Nuseirat huko Gaza yamesababisha vifo vya takriban watu 42 katika kipindi cha saa 24 huku zaidi ya nusu ya watu waliouawa wakiwa ni wanawake na watoto.

Nuseirat
Uharibifu uliotokana na shambulio la Israel katika kambi ya wakimbizi ya Nuseirat huko GazaPicha: Omar Ashtawy Apaimages/ZUMAPRESS/picture alliance

Msururu wa mashambulizi ya Israel katika kambi ya wakimbizi ya Nuseirat huko Gaza yamesababisha vifo vya takriban watu 42 katika kipindi cha saa 24 huku zaidi ya nusu ya watu waliouawa wakiwa ni wanawake na watoto. Watu wengine 150  wamejeruhiwa. Hayo ni kwa mujibu wa Marwan Abu Naser, Mkurugenzi wa hospitali ya Awda inayowapokea majeruhi.

Mashambulizi hayo yanajiri wakati Shirika la Afya Ulimwenguni likiwa limeanza tena zoezi la  kutoa chanjo ya Polio leo Jumamosi. Juhudi hizo za kuwasaidia watoto walio katika hatari zilikuwa kwenye njia panda baada ya kushudiwa kwa mashambulizi makali ya Israel.

Soma zaidi.Israel yashambulia maeneo 120 ya Hamas na Hezbollah 

Kwa upande mwingine, kundi la wapiganaji wa Hezbollah lilifanya mashambulizi ya makombora katika mji wa kati wa Israel mapema leo ambapo watu 11 walijeruhiwa.   

Hata hivyo, Mengi ya makombora hayo yalizuiwa na mfumo wa ulinzi wa anga wa Israel huku mengine yakianguka katika maeneo yasiyo na watu.