1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroIsrael

Israel yafanya operesheni ya kijeshi Jenin

Angela Mdungu Wahariri: Jacob Safari/ Bruce Amani
5 Julai 2024

Watu watano wameuwawa katika mji wa Jenin kwenye Ukingo wa Magharibi siku ya Ijumaa. Ni katika kile jeshi la Israel inachokitaja kuwa operesheni ya kupambana na ugaidi.

Gari la kivita la Israel mjini Jenin, Ukingo wa Magharibi
Jenin, Ukingo wa MagharibiPicha: Zain Jaafar/AFP

Operesheni hiyo ya Israel imejumuisha mashambulizi ya anga katika eneo hilo.Wizara ya Afya ya mamlaka ya Palestina imesema kuwa watu watano wameuwawa Ijumaa kutokana na operesheni ya Jeshi la Israel inayoendelea kwenye mji wa Jenin.

Kulingana na wizara hiyo, Wapalestina wasiopungua 12 wameuwawa ndani ya wiki hii katika eneo hilo linaloshuhudia ongezeko la machafuko tangu vita vilipoanza ndani ya Gaza mnamo mwezi Oktoba mwaka uliopita.

Kwa upande wake jeshi la Israel limesema wapiganaji wake walilizunguka jengo linalodaiwa kukaliwa na magaidi huku wakirushiana risasi. Mapambano katika mji wa Jenin panakojulikana kuwa ngome muhimu ya wanamgambo yameibuka siku moja baada ya  kundi la Israel linalopinga makazi ya walowezi  kusema kuwa serikali inapanga kujenga makazi mapya 5,300 katika eneo la walowezi katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kimabavu.

Makabiliano hayo yanaendelea wakati Shirika la Afya duniani WHO likitoa tahadhari kwamba, uhaba wa mafuta katika Ukanda wa Gaza huenda ukasababisha janga kubwa zaidi katika huduma za afya za eneo hilo ambazo ziko kwenye hali mbaya.

Jeshi la Israel, Hezbollah washambuliana

Katika hatua nyingine, kundi la Lebanon la Hezbollah lilishambulia kwa zaidi ya roketi na ndege  200 zisizo na rubani katika maeneo kadhaa ya jeshi la Israel siku ya Alhamisi.  Katika kujibu mashambulizi, jeshi la Israel nalo limechapisha picha za video zinazoonesha mashambulizi yake dhidi ya miundombinu ya Hezbollah kusini mwa Lebanon.

Juhudi za kuzima moto baada ya shambulio la Hezbolah katika eneo la milima ya Golan la IsraelPicha: Gil Eliyahu/AP Photo/picture alliance

Majibizano ya mashambulizi hayo yamezidi kupamba moto na kuendelea kuchochea mivutano kati ya pande hizo mbili wakati vita kati ya Israel na kundi la Hamas vikizidi kupamba moto.

Juhudi za mazungumzo ya usitishaji vita zaanza kuleta matumaini.

Hata hivyo juhudi za kupata makubaliano kuhusu usitishaji wa vita na kuachiliwa kwa mateka wanaoshikiliwa Gaza zimeanza kuonesha matumaini. Ni baada ya kundi la Hamas kutoa mapendekezo yaliyofanyiwa marekebisho kuhusu masharti ya makubaliano yake na Israel ikisema kuwa itaanza tena majadiliano ambayo yalikwama hapo awali.

Soma zaidi: Netanyahu kupeleka wawakilishi majadiliano ya kusitisha vita Gaza

Awali Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alimueleza Rais Joe Biden wa Marekani kuwa angetuma ujumbe ili kuendelea na mazungumzo.

Wakati hayo yakijiri, kiongozi wa kundi la Hezbollah Sayyed Hassan Nasrallah na afisa wa ngazi ya juu wa kundi la Hamas Khalil Al-Hayya wamekutana kujadili juu ya hali inayoendelea katika Ukanda wa Gaza. Wawili hao wamejadili pia kuhusu mazungumzo yanayolenga kupata makubaliano ya usitishaji vita.

Vyanzo: APE/RTR/AP/AFP/Reuters

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW