Mashambulizi ya Israel yawaangamiza 17 Gaza
17 Septemba 2025
Jeshi la Israel limesema limelenga maeneo zaidi ya 150 katika mji wa Gaza City tangu ilipoanza operesheni yake ya ardhini mjini humo hapo jana Jumanne huku ikisema imewashambulia moja kwa moja wanamgambo wa Hamas na maeneo yao muhimu ya kijeshi.
Taarifa zinazotolewa na shirika la habari la Palestina pamoja na jeshi la Israel zote hazijathibitishwa kufikia sasa.
Lakini Tume huru ya uchunguzi ya Baraza la Haki za Binaadamu la Umoja wa Mataifa imesema Israel inatekeleza mauaji ya kimbari dhidi ya wapalestina katika ukanda huo wa Gaza.
Israel imekanusha hilo la kulishutumu kundi la Hamas kwa kutekeleza mauaji hayo ya kimbari wakati iliposhambulia kusini mwa taifa hilo mnamo Oktoba 7 mwaka 2023 tukio lililochochea mgogoro uliopo sasa.
Haya yanatokea wakati wito wa kusitisha mapigano bado unaendelea kutolewa.
Kiongozi wa kanisa katoliki dunia Papa Leo XIV amekosoa hali mbaya inayowakabili wapalestina Gaza akionesha mshikamano wake na watu hao huku akirejelea wito wake wa usitishwaji wa vita kati ya Israel na Hamas.
"Ninaelezea ukaribu wangu kwa watu wa Palestina huko Gaza, wanaoendelea kuishi kwa hofu na katika mazingira yasiyokubalika, waliohamishwa tena kwa nguvu kutoka ardhi zao. Mungu aliamuru kwamba"usiue" kwa hiyo kila mtu ana haki ya kuheshimiwa. Narejelea wito wangu wa kusitishwa kwa vita, kuachiwa kwa mateka, kuwepo kwa suluhu ya kidiplomasia na sheria ya kimataifa ya haki za binaadamu kuheshimiwa kikamilifu. Namuomba kila mmoja kuungana nami katika maombi ya dhati, ili amani itawale hivi karibuni," alisema Papa Leo.
Ulaya yapendekeza vikwazo dhidi ya Israel kufuatia matendo yake Gaza
Kando na hayo hali ya kibinaadamu inayoendelea kuwa mbaya Gaza imeongeza shinikizo la kisiasa kwa viongozi wa Ulaya kuchukua hatua za kusitisha mapigano. Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya imependekeza kusimamisha kwa muda mipango ya biashara itakaoathiri takriban yuro bilioni 5.8 ya mauzo ya nje ya Israel.
Hatua hiyo imechukuliwa kufuatia operesheni hiyo ya Israel mjini Gaza. Hata hivyo mpango huo kwa sasa hauna uungwaji mkono wa kutosha wa nchi wanachama wa Umoja huo.
Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Kaja Kallas pia alipendekeza awamu nyengine ya vikwazo dhidi ya mawaziri wawili wa Israel, walowezi wanaozua vurugu na Viongozi 10 wa kundi la Hamas.
Waziri wa usalama wa Taifa wa Israel Itamar Ben-Gvir na Waziri wa fedha Bezalel Smotrich ndio walioangukiwa na vikwazo hivyo. Israel kupitia waziri wake wa mambo ya nje Gideon Saar tayari imeshatoa onyo kwa Ulaya dhidi ya kuichukulia nchi hiyo hatua akisema hilo litaathiri matakwa ya Ulaya. Amesema hatua yoyote dhidi ya Israel itakuwa na majibu makali.