1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mashambulizi ya kigaidi Kenya: Wanasiasa waonyesheana vidole

18 Juni 2014

Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya amesema mashambulizi mawili yaliyowauwa watu zaidi ya 60 kisiwani Lamu hivi karibuni hayajafanywa na kundi la Al Shabab bali na mtandao wa wanasiasa waliopo nchini humo na wahalifu.

Kenianischer Präsident Uhuru Kenyatta
Picha: picture-alliance/AA

Akiongea wakati wa hotuba yake kuhusiana na mashambulizi hayo, Rais Kenyatta amesema kuna ushahidi unaoonesha mashambulizi yalipangwa na baadhi ya wanasiasa wanaotaka kuanzisha mapigano ya kikabila dhidi ya wakenya.

Ameongeza kuwa katika siku za hivi karibuni wakenya wameshuhudia siasa chafu ambazo zinalengo la kuwafanya watu wavunje sheria pamoja na kuleta vurugu katika nchi hiyo. "Hili halikuwa shambulizi la Al Shabab, ushahidi unaonesha kuwa mtandao wa wanasiasa wa hapa nchini wanahusika katika kupanga na kutekeleza shambulizi hili la kutisha" alisema Rais Kenyatta.

Sehemu ya eneo la Mpeketoni iliyaoharibiwa na shambulizi ambalo kundi la Al-Shabaab lilidai kuhusika nalo.Picha: picture-alliance/dpa

Wapinzani wakosoa matamshi ya rais

Kufuatia kali hiyo ya Rais Kenyatta, baadhi ya wanasiasa hususani wale wa vyama vya upinzani wameikosoa kauli yake hiyo. Anyang Nyon'go ambaye ni Katibu Mkuu wa chama cha upinzani CORD, amemkosoa rais Kenyatta kwa kusema huu sio wakati wa kunyosheana vidole vya lawama bali ni wakati wa kuungana kama wakenya kuhakikisha usalama dhabiti unapatikana nchini humo.

Nyon'go hata hivyo amesema matamshi yaliyotolewa na rais Kenyatta kwa sasa yamekosa muelekeo na kumtaka kutoa ushahidi alionao dhidi ya madai ya wanasiasa kuhusika katika mashambulizi.

Kauli hiyo ya Rais Kenyatta kuyahusisha mashambulizi hayo ya hivi karibuni na mtandao wa wanasiasa nchini humo inakuja wakati ambapo kundi la Al Shabab kukiri kuhusika katika mashambulizi hayo kutokana na Kenya kushindwa kuondoa majeshi yake nchini Somalia ambayo yanaisaidia serikali ya nchi hiyo kupambana na kundi hilo la kaigaidi.

"Shambulizi la pili lilikuwa na mafanikio" alisema mmoja wa wapiganaji wa kundi la Al Shabab wakati alipokuwa anaongea na kituo cha Andalus ambacho huwa kinatumiwa mara kwa mara na kundi hilo la kigaidi.

Lakini baadhi ya wachambuzi wa masuala ya usalama wanaelezea wasiwasi wao kama ni kweli mashambulizi hayo yametekelezwa na kundi hilo, Matt Bryden ambaye ni mkuu wa zamani wa kundi la uangalizi la Umoja wa Mataifa nchini Somalia na sasa akiwa ni mkuu wa kituo cha utafiti cha Sahan anasema kuwa Al Shabab haijawahi kukiri kuhusika katika shambulizi lolote ambalo imeshawahi kufanya huku pia hakuna ushahidi wa kundi lolote la Kenya ambalo lina uwezo wa kufanya shambulizi kubwa na lenye mbinu kama zilizotumika katika mashambulizi hayo.

Kiongozi wa muungano wa upinzani wa CORD Raila Odinga.Picha: Will Boase/AFP/Getty Images

Raia wajawa na wasiwasi

Raia wengi wa Kenya wameonesha kuwa na wasiwasi na mbinu ambazo zinatumiwa na serikali katika kupambana na matukio ya kigaidi tokea litokee shambulizi katika jengo la biashara la Westgate mwaka jana.

Serikali ya nchi hiyo imeanzisha mikakati mbalimbali ya usalama ikiwemo ule wa uangalizi kati ya watu wanaoishi katika maeneo ya majirani, upigwaji marufuku wa matumizi ya magari yanayosafirisha abiria yenye vioo ambavyo havioneshi ndani lakini pia kampeni ya utoaji taarifa.

" Kenyatta anajaribu kutuambia kuwa suala la usalama ni jukumu letu, sio kweli usalama ni jukumu la serikali" alisema mmoja wa wanaharakati nchini humo Boniface Mwangi.

Kumekuwepo pia na taarifa ya kufukuzwa kazi au kuhamishwa kwa maafisa wa polisi wa Mpeketoni ambako ndipo shambulizi moja lilitokea na kufuatiwa na lile la kijiji cha Poromoko, lakini baadhi ya raia wa Kenya wanakasirishwa na kitendo cha serikali ya nchi hiyo kuwaacha maafisa wa juu wa polisi ambao wameteuliwa kisiasa.

Mwandishi: Anuary Mkama/dpa, ap
Mhariri:Yusuf Saumu

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi