Mashambulizi ya mabomu yauwa watu 46 Iraq
15 Januari 2014Matukio haya mawili yanayoirejesha nyuma serikali ya Iraq katika mapambano yake ya kuidhibiti nchi, yanakuja miezi kadhaa kabla ya kufanyika uchaguzi wa bunge.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, amewahimiza viongozi wa Iraq kutafuta suluhu ya kisiasa ya kusimamisha ghasia zinazoonekana kusambaa katika maeneo mengi nchini humo. Hata hivyo Waziri Mkuu Nuri al-Maliki ameondoa uwezekano wa kuzungumza na wanamgambo kwa kuwa vikosi vyake vimeanzisha operesheni kali dhidi yao.
Hata hivyo, operesheni hiyo ambayo serikali inasema imesababisha kuuwawa na kutiwa nguvuni kwa wanamgambo wanaofungamanishwa na kundi la kigaidi la Al Qaida, bado haijafanikiwa kusimamisha umwagikaji damu nchini humo.
Mashambulizi yalenga maeneo yaliojaa watu
Magari saba yaliyojazwa mabomu yaliwekwa katika maeneo yaliyojaa waumini wa madhehebu ya Shia, mengine yaliegeshwa kwenye masoko yaliojaa watu mjini Baghdad na mengine kuwekwa karibu na mkahawa mmoja katika barabara ya Sanaa. Yote yaliripuka na kusababisha mauaji ya watu 24.
Kulingana na mwandishi habari wa shirika la AFP mripuko uliotokea katika Barabara ya Sanaa ulisababisha mauaji ya watu watatu huku mkahawa uliolengwa ukiharibika vibaya pamoja na magari yaliyokuwa karibu wakati wa mashambulizi hayo
Kwengineko mshambuliaji wa kujitoa muhanga katika mazishi mjini Buhruz, kaskazini mwa Baghdad, aliuwa watu 16 na wengine zaidi ya 20 kujeruhiwa. Mazishi hayo yalikuwa ya mwanachama wa kundi la Sahwa mwanamgambo kutoka madhehebu ya Sunni aliyekuwa karibu na jeshi la Marekani mwaka wa 2008 dhidi ya al-Qaida akiwasaidia katika kudhibiti uasi.
Mpaka sasa hakuna kundi lolote lililodai kuhusika na mashambulizi hayo lakini wanamgambo wa Kisunni wanaoshirikiana na wale wa Kundi la Dola ya Kiislamu ya Iraq na Sham, ISIL, wanashukiwa kupanga mashambulizi hayo pamoja dhidi ya wapiganaji wa Sahwa.
Kwa sasa Waziri Mkuu Nuri al-Maliki ameomba hatua ya pamoja ya kimataifa dhidi kundi la al-Qaida na washirika wake.
Hii ni mara ya kwaza kwa wanamgambo kuwa na udhibiti wa hali ya juu katika miji mikubwa tangu uasi uliosababishwa na jeshi la Marekani kuivamia Iraq mwaka wa 2003.
Mwandishi: Amina Abubakar/AFP
Mhariri: Mohammed helef