1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroNigeria

Mashambulizi ya magenge yauwa watu 160 katikati mwa Nigeria

26 Desemba 2023

Idadi ya watu waliopoteza maisha katika mfululizo wa mashambulizi ya magenge ya watu wenye silaha yaliyovilenga vijiji kadhaa katikati mwa Nigeria imepanda na kufikia 160.

Afisa usalama wa Nigeria
Ukosefu wa usalama unaotokana na makundi ya watu wenye silaha na yale ya itikadi kali uiandama Nigeria kwa miaka kadhaa sasa. Picha: Christina Aldehuela/AFP/Getty Images

Hayo yameelezwa na viongozi kwenye wilaya za jimbo la Plateau ambako matukio hayo ya kulengwa vijiji yametokea. Taarifa zinasema watu wenye silaha walivamia vijiji visivyopungua 20 kwenye wilaya ya Bokkos, wakawashambulia watu na kuwauwa 113 na kuzichoma moto nyumba wenye maeneo hayo.

"Tumewakuta watu zaidi ya 300 wamejeruhiwa" amesema Monday Kasah, kiongozi wa serikali katika wilaya ya Bokkos. Amesema wote wamepelekwa kwenye hospitali za wilaya hiyo, wengine kwenye mji mkuu wa jimbo hilo, Jos, na wengine kwenye wilaya jira ya Barkin ladi.

Kwenye wilaya jirani ya Barkin Ladi watu wengine wapatao 50 wameuwawa katika mkururo huo mashambulizi hayo ya magenge ya wahuni. 

Mashambulizi huenda yamechochewa ni chuki za kidini au makabila 

Njia ya kuingia mji mkuu wa jimbo la Plateau, Jos.Picha: Kola Sulaimon/AFP/Getty Images

Takwimu hizo ni kulingana na Dickson Chollom ambaye ni mwakilishi kwenye Bunge la Jimbo zima. Amelaani mashambulizi hayo na kuvitolea mwito vyombo vya usalama kuchukua hatua madhubuti.

"Hatutasalimu amri mbele ya mbinu za hawa mawakala wa kifo. Tuko imara kwenye kutafuta haki na amani ya kudumu, " amesema Chollom.

Gavana wa jimbo la Plateau Caleb Mutfwang naye pia amelaani mauaji hayo akiyataja kuwa ya "kinyama na udhalimu mkubwa."

Inaaminika kuwa mauaji hayo huenda yamechochewa na chuki za kidini au kikabila. Jimbo la Plateau linafahamika kwa mizozo ya kila wakati hususani baina ya jamii ya wafugaji ambao wengi ni waislamu dhidi ya wakristo ambao wengi ni wakulima. Gavana Mutfwang amesema serikali itachukua hatua za mapema kuzuia matukio kama hayo kutokea tena.

Hadi jana Jumatatu, milio ya risasi ilikuwa bado inasikika. Mkaazi mmoja wa kijiji cha Mushu ameliambia Shirika la Habari la AFP kwamba walikuwa wamelala usiku wa manane kuamkia Jumapili ndipo walisikia milio ya risasi na washambuliaji waliwauwa na kuwajeruhi baadhi ya wanakijiji na kuwateka nyara wengine.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW