Urusi yaishambulia Ukraine kwa makombora, droni
15 Januari 2025Kupitia mitandao ya kijamii Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amesema kando ya makombora yaliyorushwa nchini mwake, Urusi ilishambulia pia kwa kutumia ndege 70 zisizo na rubani usiku wa kuamkia Jumatano.
Kwa upande wake Waziri wa Nishati wa Ukraine, Herman Halushchenko ameeleza kuwa mashambulizi hayo ya Urusi yameilazimu mikoa sita ya nchi hiyo kuingia katika mgao wa umeme wa dharura kama hatua ya kujihami wakati taifa hilo likikabiliwa na kile mamlaka zilichokitaja kuwa mashambulizi makubwa ya Urusi. Kupitia ukurasa wake wa Facebook, Halushchenko amewataka raia waingie katika maeneo maalumu yenye kinga dhidi ya mabomu mara wanaposikia ving'ora vya tahadhari dhidi ya mashambulizi ya anga.
Soma zaidi: Urusi yadai kuviteka vijiji viwili mashariki mwa Ukraine
Gavana wa Mkoa wa Ivano Frankivsk, amesema miundombinu muhimu ililengwa katika eneo la Prykarpattia, hata hivyo hakuna watu waliojeruhiwa na na hali katika eneo hilo imedhibitiwa.
Mamlaka za jimbo la Lviv linalopakana na Poland zimeeleza pia kwamba miundombinu miwili muhimu imeshambuliwa katika wilaya mbili. Zimesema licha ya mashambulizi hayo hakuna majeruhi, lakini kuna uharibifu wa mali.
Zelensky ziarani Poland
Mashambulizi ya Urusi dhidi ya Ukraine yamefanywa wakati Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky akitarajiwa kuwasili nchini Poland Jumatano kwa ajili ya kufanya mazungumzo na Waziri Mkuu Donald Tusk mjini Warsaw. Ziara hiyo inafanyika siku kadhaa baada ya Waziri Mkuu Tusk kutangaza kuwa wamepiga hatua juu ya mvutano unaotokana na mauaji ya raia wa Poland yaliyofanywa na raia wa Ukraine wakati wa Vita vya Pili vya Dunia.
Mazungumzo ya wawili hao yanafanyika siku chache kabla ya kuapishwa kwa Donald Trump kuwa rais wa Marekani.
Trump ambaye ni mwanachama wa chama cha Republican ameahidi kuumaliza mara moja mzozo kati ya Urusi na Ukraine atakapoingia madarakani, hali inayozua hofu kwa Ukraine kuwa huenda akailazimisha kuiachia Urusi sehemu ya maeneo yake ili amani irejee.
Wakati huo huo, Ujerumani inapanga kuipa Ukraine makombora mengine 60 aina ya IRIS-T ili iimarishe ulinzi wa anga dhidi ya mashambulizi ya Urusi. Uamuzi huo umefanyika baada ya Waziri wa Ulinzi Boris Pistorius kuitembelea Kyiv ambako alifanya mazungumzo na Rais Zelensky.