Mashambulizi ya NATO yauwa raia Afghanistan
29 Mei 2011Msemaji wa serikali ya Afghanistan, amesema shambulizi hilo katika Wilaya ya Nawzad, lilifanywa baada ya wanajeshi wa Marekani kushambuliwa na kundi la Taliban. Hapo jana, Rais wa Afghanistan Hamid Karzai, aliiamuru Wizara ya Ulinzi kuchukua udhibiti wa mashambulizi yote ya usiku na kuyazuia majeshi ya kigeni kufanya mashambulizi yasiyoratibiwa.
Wakati huo huo wanajeshi wawili wa Ujerumani na afisa mmoja wa polisi wa ngazi ya juu wa Afghanistan, wameuawa katika shambulizi la kujitoa muhanga, lililotokea katika mkoa wa Takhar nchini Afghanistan hapo jana.
Kamanda wa vikosi vya jumuiya ya kujihami ya NATO kaskazini mwa Afghanistan, jenerali wa Kijerumani Markus Kneip, alinusurika kwa kupata majeraha madogo. Wanajeshi wengine wanne wa Ujerumani, walijeruhiwa katika shambulizi hilo. Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani Thomas de Maziere, amewasifu wanajeshi hao na amewaomba Wajerumani kuendelea kuunga mkono jitahada za nchini Afghanistan.