IS yadai kuhusika katika mashambulizi ya Paris
14 Novemba 2015Katika taarifa iliyoitoa hii leo kundi hilo la wanamgambo limesema wapiganaji wake wanane waliokuwa wamevalia mikanda ya viripuzi na bunduki za rashasha walifanya mashambulizi hayo ya jana usiku katika maeneo mbali mbali katika mji mkuu wa Ufaransa baada ya kuuchunguza kwa makini.
IS imesema mashambulizi hayo ya Paris yalilenga kuionyesha Ufaransa kuwa itasalia kulengwa iwapo itaendelea na sera zake za kuwashambulia wanamgambo wa IS.
Hollande asema IS imehusika
Rais wa Ufaransa Francois Hollande amesema kundi hilo la IS limehusika katika mashambulizi ya Paris aliyoyataja mabaya zaidi kuwahi kuikukmba Ufaransa katika kipindi cha miongo kadhaa. Rais wa Syria Bashar al Assad amesema mashambulizi hayo yamechochewa na sera za Ufaransa. Ufaransa imekuwa ikishiriki katika mashambulizi ya angani dhidi ya IS nchini Iraq na Syria.
Wakati huo huo vyombo vya habari nchini Ujerumani vimeripoti hii leo kuwa mwanamume mmoja aliyekamatwa kusini mwa Ujerumani wiki iliyopita alikuwa na silaha zikiwemo bunduki za rasha rasha na viripuzi katika gari lake na kuna uwezekano huenda alihusika na mashambulizi hayo ya Paris.
Polisi katika jimbo la Bavaria imethibitisha kukamatwa kwa mtu huyo mnamo tarehe tano mwezi huu lakini imekataa kuthibitisha iwapo anahusishwa na shambulizi la Paris ambalo limesababisha mauaji ya kiasi ya watu 127.
Waziri mkuu wa Ubelgiji Charles Michel amewahimiza raia wa nchi yake kuepuka kusafiri kuelekea Paris hadi pengine iwe kuna haja kubwa mno ya kufanya hivyo.
Poland imesema haitawakubali wahamiaji chini ya makubaliano ya Umoja wa Ulaya ya nchi wanachama kugawana wahamiaji baada ya mashambulizi hayo ya Paris.
Usalama waimarishwa
Waziri wa uchukuzi wa Urusi Maxim Sokolov amesema wizara yake itatekeleza hatua za kiusalama katika sekta ya uchukuzi kote nchini Urusi baada ya mashambulizi ya Paris yanayodaiwa kufanywa na IS. Urusi inatafakari kudhibiti usafiri wa ndege kutoka Moscow hadi Paris.
Jumuiya ya kimataifa imeendelea kulaani mashambulizi hayo. Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa Francis ameyalaani mashambulizi hayo na kusema ametiwa uchungu na vifo vya waliouawa katika mashambulizi hayo aliyoyataja kitendo cha kinyama.
Maeneo ya umma Paris yamefungwa kama sehemu ya tahadhari za kiusalama huku maafisa wa usalama wakiendelea na uchunguzi.
Rais Hollande ametangza siku tatu za maombolezi nchini humo na Ujerumani pia imetangaza bendera kote nchini zitapeperushwa nusu mlingoti kama ishara ya kusimama na Ufaransa wakati huu wa majonzi.
Mwandishi: Caro Robi/afp/Reuters/dpa
Mhariri: Yusra Buwahyid