1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mashambulizi ya sumu yauwa watu 58 Syria

4 Aprili 2017

Shirika la uangalizi wa haki za binaadamu nchini Syria linasema ndege za kivita zimefanya shambulio linaloshukiwa kuwa na sumu na kuuwa watu wasiopungua 58, wakiwemo watoto kadhaa.

Syrien Idlib Giftgas Angriff
Watoto wakitibiwa katika hospitali baada ya shambulizi la ndege linaloshukiwa kuwa la kemikali katika mji wa Khan Shykhun mkoani Idlib, Aprili 4.2017Picha: picture alliance/dpa/M.Karkas

Shirika la uangalizi wa haki za binaadamu la Syria lenye makao yake mjini London Uigereza limesema waliouawa katika mji wa Khan Sheikhun katika mkoa wa Idlib, walifariki kutokana na athari za gesi, na kuongeza kuwa wengine kadhaa walikumbw ana matatizo ya kupumua na dalili nyingine.

Shirika hilo halikuweza kuthibitisha  aina ya kemikali iliotumiwa na limesema haikuwa bayana iwapo ndege zilizoshiriki katika shambulio hilo zilikuwa za Syria au mshirika wake Urusi.

Wafadhili wakutana kukusanya misaada

Shambulio hilo linakuja mwanzoni mwa mkutano wa siku mbili kuhusu mustakabali wa Syria, ulioandaliwa mjini Brussels kwa ushirikiano wa Umoja wa Ulaya na Umoja wa Mataifa. Shirika hilo la uangalizi wa hali za binadamu limesema duru kutoka mji ulioshambuliwa zimeripoti dalili miongoni mwa waahtirika zikiwemo kuzimia, kutapika na kutokwa na mapovu mdomoni.

Mwanaume akitibiwa hospitalini baada ya shambulio linaloshukiwa kuw ala kemikali mjini Khan Shaykhun, mkoani Idlib, April 4, 2017.Picha: picture alliance/dpa/M.Karkas

Waathirika wengi walikuwa raia, limesema shirika hilo na kuongeza kuwa miongoni mwao ni watoto wasiopungua tisa. Picha zilizosambazwa na wanaharakati zimewaonyesha wafanyakazi wa kujitolea wa kundi la uokozi la White Helmets wakitumia mabomba ya maji kuwaosha majeruhi, na pia wanaume wasiopungua wawili wakiwa na mapovu mdomoni.

Mkoa wa Idlib unadhibitiwa kwa sehemu kubwa na muungano wa waasi wakiwemo wahsirika wa zamani wa kundi la Al-qaeda - Fateh al-Sham. Mkoa huo hulengwa mara kwa mara na mashambulizi ya utawala wa Assad na pia ndege za kivita za Urusi, na umeshambuliwa pia na ndege za muungano unaoongozwa na Marekani unaopambana na kundi linalojiita Dola la Kiislamu IS, mara nyingi zikiwalenga wapiganaji wa kundi hilo.

Shambulio la Jumanne limekuja siku chache baada ya majeshi tiifu kwa rais Bashra al-Assad kushutumiwa kwa kutumia sila za kemikali katika mashambulizi ya kujibu katika mkoa jirani wa Hama. Siku ya Alhamisi, mashambulizi kadhaa ya angani katika maeneo kadhaa ya mkoa wa Hama yaliwasababishia karibu watu 50 matatizo ya kupumua, kulingana na shirika hilo la haki za binaadamu, ambalo halikuweza kuthibitisha sababu ya dalili hizo.

Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Nikki Haley amesema Assad ni mhalifu wa kivita na kwamba Marekani haina na mapenzi na kiongozi huyo.Picha: picture-alliance/EuropaNewswire/L. Rampelotto

Marekani: Assad ni mhalifu wa kivita

Zaidi ya watu 320,000 wameuawa nchini Syria tangu mgogoro huo ulipoanza Machi 2011 kwa maandamano ya kupingia serikali. Marekani ambayo ilikuwa ikiongoza harakati za kumuondoa Bashar al-Assad ilisema kipaumbele chake kwa sasa siyo tena kumuondoa Assad bali kupambana na makundi ya kigaidi, lakini balozi wake katika Umoja wa Mataifa Nikki Haley ambaye ndiye rais wa baraza la usalama kw amwezi wa Aprili, alisema Jumatatu kuwa hawana mpango wa kusihrikiana na kiongozi huyo.

"Hatuna mapenzi na Assad. Hilo tumeliweka wazi kabisaa. Tunaamini amekuwa kikwazo kwa amani kwa muda mrefu. Nadhani ni mhalifu wa kivita na alichowafanyia watu wake kinachukiza, na hivyo tunachojaribu kufanya ni kusema tunalishughulikiaje hili?" alisema Haley mjini New York.

Mkutano wa leo mjini Brussels umelezwa kuwa ni ufuatiliaji wa mkutano mwingine wa wafadhili uliofanyika mwaka uliopita mjini London, ambao ulikusanya karibu dola bilioni 11 kwa ajili ya programu za misaada ya kibinadamu katika nchi hiyo ilioharibiwa vibaya na vita.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/afpe.rtre, ape

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman