Mashambulizi ya Urusi yawaacha wengi bila umeme, Ukraine
28 Novemba 2024Afisa Mkuu mtendaji wa kampuni ya nishati ya Yasno nchini Ukraine, Sergey Kovalenko amesema kuna hali ya dharura ya kukatika umeme kote nchini kutokana na shambulizi la adui kwenye sekta ya nishati.
Shambulizi hilo la pamoja la kombora na droni, lililofanywa kwa awamu saa za alfajiri, lilikata umeme na kuathiri zaidi ya wateja milioni moja magharibi mwa Ukraine.
Viongozi wa NATO wajadili kuimarisha utengenezaji silaha Ukraine
Kiongozi wa mkoa wa Lviv, Maksym Kozytskyi amesema mpaka sasa, watu 523,000 hawana umeme. Mkoa wa magharibi, unaopakana na Poland ambayo ni mwanachama wa Umoja wa Ulaya na NATO, umeepushwa na mapigano makali ya uvamizi wa Urusi wa karibu miaka mitatu.
Hata hivyo umelengwa katika mashambulizi ya mara kwa mara ya makombora na droni ya Urusi. Watu wengine 280,000 wameachwa bila umeme katika mkoa wa magharibi wa Rivne, na wengine 215,000 eneo la kaskazini magharibi la Volyn, linalopakana pia na Poland.