1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIsrael

Israel na Palestina zakaribia ukingo wa kuzuka mapigano

28 Januari 2023

Kijana wa Kipalestina mwenye umri wa miaka 13 amewashambulia kwa risasi na kuwajeruhi watu wawili mjini Jerusalem siku ya Jumamosi.

Palästina I Palästinenser stoßen in Dschenin mit israelischen Truppen zusammen
Picha: Zain Jaafar/AFP/Getty Images

Walioshambuliwa ni baba na mtoto wake wa kiume na shambulizi hilo limetokea saa chache baada ya mtu mwengine mwenye bunduki kuwaua watu saba nje ya jengo la Sinagogi mjini Jerusalem.

Tukio hilo la kuuliwa watu saba linatajwa kuwa mkasa mbaya zaidi kuwahi kutokea kwa miaka mingi eneo hilo.

Mashambulizi hayo mawili yanaakisi kutanuka upya kwa mzozo kati ya Israel na Palestina licha ya miito ya Jumuiya ya Kimataifa ya kuwepo utulivu.

Polisi ya Israel imesema shambulizi la hii leo Jumamosi lilitokea majira ya asubuhi huko kwenye kitongoji cha Silwan nje kidogo ya mji wa Jerusalem Mashariki ulionyakuliwa kwa mabavu na Israel.

Baba mmoja mwenye umri wa miaka 47 na mtoto wake wa kiume mwenye miaka 23 wamepata majeraha mwilini na tangu wakati huo wanapatiwa matibabu hospitali.

Watu kadhaa wakamatwa juu ya shambulizi kwenye sinagogi

Polisi imesema imewakamata watu 42 kuhusiana na shambulizi la kwenye Sinagogi lililotokea siku ya Ijumaa.

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alipolizuru eneo la sinagogi ambako watu 7 waliuwawa na mshambuliaji wa Kipalestina Picha: Ronen Zvulun/REUTERS

Kisa hicho kilitendwa na kijana wa Kipalestina mwenye umri wa miaka 21 ambaye ni mkaazi wa Jerusalem Mashariki. Alisafiri kutoka kwenye mji huo hadi katika sinagogi la Neve Yaakov na kufyetua risasi katika siku ya sabato ya kiyahudi iliyoangukia siku ya kumbukumbu ya mauaji ya halaiki ya wayahudi "Holocaust".

Shambulizi hilo limetokea wakati mivutano inaongezeka kwenye kanda hiyo kwa kiwango kinachoibua wasiwasi. Siku ya Alhamisi jeshi la Israel lilifanya uvamizi kwenye maeneo ya Ukingo wa Magharibi uliosababisha vifo vya Wapalestina kadhaa.

Wakati waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alipolizuru eneo la mkasa wa Sinagogi umma uliokuwepo karibu ulipaza sauti ukisema "kifo kwa waarabu".

Wapalestina waandamana kusifu mashambulizi huku viongozi wa mataifa kadhaa wakiyalaani 

Huko Ukanda wa Gaza na Ukingo wa Magharibi, Wapalestina nao walishangilia mauaji dhidi ya Waisrael. Mjini Ramallah kulikuwa na kusanyiko kubwa la watu walioteremka mitaani wakionesha furaha na kupeperusha bendera za Palestina.

Mkuu wa polisi ya Israel imesema Kobi Shabtai amelitaja shambulizi hilo kwenye sinagogi kuwa "moja ya mashambulizi mabaya kabisa nchini israel kuwahi kutokea miaka ya karibuni".

Picha: Ahmad Gharabli/AFP/Getty Images

Mataifa kadhaa ya kiarabu yenye mahusiano na Israel -- ikiwemo Misri, Jordan na Umoja wa Falme za Kiarabu -- wamelaani shambulizi hilo la siku ya Ijumaa.

Hata hivyo kundi la Hezbollah la nchini Lebanon, moja ya mahasimu wakubwa wa Israel wamelisifu shambulizi la kwenye sinagogi kama la "kishujaa" na kuonesha uungaji mkono wa wazi kwa Palestina.

Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz amesema "ameshtushwa sana" na mashambulizi "mabaya" mjini Jerusalem na kwamba nchi yake "inasimama upande wa Israel".

Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa amesema "wimbi la machafuko ni sharti liepukwe kwa gharama zozote".