Mashambulizi zaidi nchini Nigeria
23 Desemba 2014Bomu moja lililotegwa ndani ya gari liliripuka katika kituo cha basi mjini Gombe. Kulingana na afisa mmoja wa shirika la msalaba mwekundu katika eneo hilo Abubakar Yakubu, watu 20 waliuwawa huku wengine 60 wakijeruhiwa.
Yakubu ameongeza kuwa wale waliopoteza maisha waliungua kiasi cha kutotambulika. Naibu msimamizi wa polisi Fwaje Atajiri, amesema mripuko wa Gombe umetokea wakati watu walipokuwa katika pirika pirika za usafiri kwa likizo za mwezi wa Desemba.
Kwa upande wake Kamishna wa Afya Sani Malami amesema katika jimbo jirani la Bauchi Magharibi mwa Gombe mripuko uliotokea sokoni ulisababisha mauaji ya watu sita huku wengine 19 wakijeruhiwa.
Hata hivyo hakuna mtu yeyote aliyejitokeza kukiri kuhusika na mashambulizi hayo yaliotokea hapo jana jioni, lakini walioshuhudia wanasema mashambulizi yamefanywa kwa namna ile ile wanamgambo wa Boko Haram wanavyoendesha mashambulizi yao.
Huku hayo yakiarifiwa katika shambulizi lililotokea mapema kabla ya mashambulizi hayo mawili, inasemekana mshambuliaji alisema ''Allahu Akbar'' yaani mungu ni mkubwa kisha akaendesha gari lake hadi mji wa Kakazini Mashariki wa Geidan ulioko mjini Yobe na kuanza kuwamiminia risasi wakaazi wa eneo hilo.
Washambuliaji waharibu minara ya mawasiliano ya simu
Musa Isa afisa wa polisi katika eneo hilo amesema washambuliaji waliharibu minara ya mawasiliano ya simu na kuuwacha mji huo bila mawasiliano. washambuliaji hao pia wanasemekana kuvamia gereza moja mjini humo na kuwaachia huru wafungwa, kando na hilo walirusha mabomu yaliyochoma na kuharibu vituo vya polisi, majengo ya serikali na magari ya polisi.
Wanamgambo walio na itikadi kali wa Boko Haram wanataka kuifanya Nigeria kuwa dola la kiislamu. Wakazi wengi wa nchi hiyo kwa upande wa kaskazini ni waislamu, huku upande wa kusini ukikaliwa hasa na wakristo. Mwaka huu wa 2014 Mamia ya wanigeria wameuwawa kwa mabomu na waripuaji wa kujitoa mhanga hasaa Kaskazini Mahshariki mwa nchi ambako ni ngome ya wanamgambo walio na itikadi kali.
Baadhi ya mashambulizi mabaya zaidi ni pamoja na mashambulizi mawili ya pamoja mjini Jos yaliowauwa watu 118 mwezi Mei mwaka huu, shambulizi jengine ni mripuko wa bomu uliotegwa ndani ya gari na kusababisha mauaji ya watu 100 mjini Abuja mwezi Aprili mwaka huu, shambulizi jengine ni lile la mripuaji wa kujitolea muhanga aliyewauwa watu wanafunzi 58 katika shule moja mjini Potiskum katika jimbo la Yobe pamoja na shambulizi lililofanywa na ndani ya msikiti hivi karibuni Kaskazini mwa mji wa Kano mji wa pili kwa ukubwa nchini Nigeria, shambulizi lililosababisha mauaji ya watu 120.
Mwandishi Amina Abubakar/AP/Reuters
Mhariri Daniel Gakuba