1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mashariki ya Kati yaadhimisha Eid, vita vikirindima

20 Machi 2026

Afrika Mashariki inaendelea na mfungo wa Ramadhan huku Mashariki ya Kati katika mataifa kama Saudia Arabia wakisherehekea sikukuu ya Eid al-Fitr katikati mwa vita vya Iran.

Wapalestina wakifanya manunuzi ya Eid
Wapalestina wakifanya manunuzi ya EidPicha: Matar Al-Zaq/APAimages/IMAGO

Mataifa ya Ghuba yametangaza kuwa sala za sikukuu ya Eid mwaka huu zitafanyika katika misikiti ya kawaida badala ya umati wa watu kukusanyika viwanjani kama ilivyo ada, hiyo ikiwa ni tahadhari tu kutokana na mashambulizi yanayofanywa na Iran kwa mataifa hayo.

Wapalestina katika Ukanda wa Gaza ulioharibiwa vibaya na vita leo wamekusanyika kuadhimisha sikukuu ya Iddi inayoashiria mwisho wa mwezi wa mfungo wa Ramadhan.

Wakiwa wamedhamiria kukiondoa kiwingu kilicholetwa na vita katika ukanda huo, wazazi katika eneo la Khan Younis walikusanyika kuoka biskuti kwa ajili ya watoto wao ambao maisha yao yameathirika vibaya na vita.

Huku mapigano makali yakiwa yamepungua huko Gaza kutokana na makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyofikiwa, Israel imekuwa ikifanya mashambulizi ya hapa na pale kila kukicha.

Mazingira ya maadhimisho ya Eid yabadilika

Huko nchini Irak katika mji wa Erbil nako, maandalizi ya sherehe hizo yanafanyika ila kwa kasi ndogo huku wasiwasi wa usalama ukiwa umewagubika raia kutokana na vita vya Iran, Marekani na Israel.

Wamiliki wa maduka katika mji huo wanasema mazingira yamebadilika katika sherehe za mwaka huu ikilinganishwa na sherehe za mwaka jana. Licha ya wasiwasi ulioko, masoko yamesalia wazi huku familia zikiendelea kufanya manunuzi kwa ajili ya sherehe hizo za Eid.

Wapakistani wakiabiri treni kwenda vijijini kusherehekea EidPicha: Munir Uz Zaman/AFP

Tangu kuanza kwa vita vya Iran mnamo Februari 28, Irak imeshuhudia mashambulizi kadhaa yakiwemo ya droni na makombora kufanywa nchini humo huku kambi za kijeshi, miundo mbinu ya mafuta na maeneo mengine yakishambuliwa.

Nako nchini Afghanistan waumini wa Kiislamu wameadhimisha sikukuu ya Iddi kwa sala katika msikiti wa Sha-Do Shamshira. Mapema Jumatano, Afghanistan na Pakistan walitangaza usitishwaji wa mapigano yanayozidi baina ya nchi hizo mbili, siku mbili baada ya Kabul kuilaumu Islamabad kwa shambulizi la angani katika mji huo mkuu, lililosababisha vifo vya mamia ya watu.

Nchi hizo mbili zimetangaza kwa pamoja kuwa zinasitisha vita kupisha sherehe za Iddi kutokana na mwito wa Saudi Arabia, Uturuki na Qatar.

Huko Pakistan nako sikukuu hiyo inaadhimishwa Alhamis huku maelfu ya watu wakiwa wamefurika kwenye vituo vya mabasi na treni huko Lahore kujaribu kupata usafiri kuelekea maeneo ya vijijini kwa ajili ya kusherehekea na familia zao.

Hali ni sawa na hiyo huko nchini India na Bangaldesh ambako Waislamu wanaadhimisha sherehe hiyo baada ya mwezi wa Ramadhan, ila sherehe za mwaka huu zimegubikwa na vita vinavyoendelea nchini Iran, ambavyo vimesababisha kuongezeka kwa bei za mafuta na gesi.

Katika Mji Mkuu wa India New delhi, uhaba wa mitungi ya gesi inayotumiwa na wengi kwa mapishi, ni jambo lililosababisha migahawa mingi kutumia meko yanayotumia mkaa, kuandaa vyakula vya sikukuu.

Serikali ya India imechukua hatua ya kuelekeza mitungi mingi zaidi ya gesi kutumika majumbani badala ya migahawa na mahotelini. Bei za bidhaa nchini humo zimepanda, na baadhi ya migahawa imechukua hatua ya kutopika baadhi ya vyakula kutokana na matatizo hayo ya nishati, ambayo yamesababishwa pakubwa na vita vya Iran.

India kwa sehemu kubwa inategemea gesi na mafuta yanayosafirishwa kupitia mlango bahari wa Hormuz.

Iran kuadhimisha Eid Jumamosi

Haya yanafanyika wakati ambapo Iran imetangaza kuwa leo Ijumaa ndiyo siku ya mwisho ya mfungo wa Ramadhan huko taifa hilo lililo na idadi kubwa ya Waislamu wa Kishia likitangaza kuwa sherehe za Eid zitafanyika Jumamosi.

Kiongozi mkuu wa Iran Ayatollah Mojtaba KhameneiPicha: Sha Dati/Xinhua/IMAGO

Taarifa hiyo imetolewa na ofisi ya kiongozi mkuu wa Mojtaba Khamenei ikisema kuwa Ijumaa ndiyo itakayokuwa siku ya 30 na itakuwa pia siku ya kutazama kuandama kwa mwezi, kulingana na kalenda ya Kiislamu.

Mwaka huu, siku ya mwisho ya Ramadhan huko nchini Iran, inakuja wakati wa sherehe za mwaka mpya wa Nowruz.

Katika mwezi mtukufu wa Ramadhan mamilioni ya Waislamu kote duniani hufunga kuanzia alfajiri hadi magharibi, hiyo ikiwa moja ya nguzi tano za Uislamu, ambapo waumini wanatakiwa kutokula, kunywa, kuvuta sigara na kutoshiriki ngono wakati wakiwa kwenye saumu.

Katika kipindi hicho, Waislamu hutakiwa pia kutoa zaka kwa maskini. 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW