Mashindano ya Baiskeli yashika kasi Rwanda
22 Septemba 2025
Bingwa mara nne wa Tour de France alikuwa akilenga kutwaa mataji mawili — muda binafsi na mbio za barabarani — lakini alishindwa waziwazi na Mbelgiji Remco Evenepoel katika mbio za muda binafsi zilizoanza mashindano hayo ya wiki moja mjini Kigali.
Pogacar alikuwa wa pili kutoka mwisho kuanza mbio za kilomita 40.6, akifuatiwa na Evenepoel ambaye alimshinda kwa kumzidi kwa takriban kilomita 2 kabla ya kumaliza na kutwaa taji lake la dunia kwa mara ya tatu mfululizo.
Pogacar alisema "Aliponipita nilisema tu 'wow'. Kupata dakika mbili na nusu ni jambo la ajabu. Hongera kwa Remco." "Siyo hisia nzuri unapopitwa na mwanariadha, lakini yeye ndiye bora katika mbio hizi. Anawekeza muda mwingi, na mimi naweza tu kutumaini kumkaribia miaka ijayo."
"Nilitaka kufanya vyema zaidi na kuwa katika na nafasi ya kushinda mataji yote mawili wiki hii, lakini kwa bahati mbaya sikupata mwendo mzuri. Labda sikufanya mazoezi ya kutosha kujiandaa, baada ya kuungua mwezi uliopita.
"Nilifika hapa nikiwa na ari ya juu, lakini nilipaswa kuwa na nguvu za kipekee — jambo ambalo sikuweza kutimiza," aliongeza.
Sasa Pogacar ana wiki moja ya kujiimarisha kabla ya kushiriki mbio kuu za barabarani Jumapili(28.09.2025), ambazo zitafunga rasmi mashindano ya dunia ya kwanza kufanyika barani Afrika.
Mbio hizo zitakuwa na urefu wa kilomita 267.5, zenye mwinuko wa zaidi ya mita 5,500 — kiwango cha pili cha juu zaidi katika historia ya Mashindano ya Dunia ya Mbio za Barabarani.
Marlen Reusser atamba kwa Wanawake
Mshindi wa fedha katika mashindano ya Tokyo, Marlen Reusser kutoka Uswisi, alitwaa taji lake la kwanza la muda binafsi kwa wanawake. Alikamilisha mbio za kilomita 31.2 kwa muda wa dakika 43 na sekunde 09.34.
Anna van der Breggen kutoka Uholanzi aliongoza kwa muda mrefu lakini alishika nafasi ya pili, sekunde 51.89 nyuma ya Reusser, huku Demi Vollering akichukua shaba.
Reusser amekuwa akisubiri kwa muda mrefu kushinda dhahabu katika mbio hizi baada ya kushinda fedha kwenye Olimpiki ya Tokyo 2020 na kupata medali mbili za fedha na moja ya shaba kwenye mashindano ya dunia.
"Ninahisi kama nimepanda jukwaani mara kumi. Siwezi hata kuamini," alisema.
"Najua ni kweli na limetokea, lakini nilijaribu mara nyingi na sikufanikiwa. Na sasa, naamini nimefanikiwa, na ni jambo la kipekee sana — lakini ilihitaji juhudi kubwa."
Mivutano ya Kisiasa Yazua Maswali Kuhusu Mashindano Rwanda
Huku mashindano haya yakifanyika kwa mara ya kwanza Afrika, wasiwasi kuhusu usalama, mijadala ya kisiasa na kutokuwepo kwa nyota wengi wa mbio za baiskeli vimetia doa mashindano ya mwaka huu.
Uamuzi wa kuandaa mashindano Rwanda umekuwa tata tangu mwanzo, huku makundi ya haki za binadamu yakimtuhumu Rais Paul Kagame kwa kutumia michezo kuisafisha taswira ya nchi ("sportswashing").
Bunge la Umoja wa Ulaya limeiwekea Rwanda vikwazo mwaka huu kwa kuunga mkono kundi la waasi la M23 nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, na baadhi ya wabunge walitaka mashindano hayo yafutwe.