1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mashirika ya haki za binadamu yaomba uchunguzi huru Goma

Saleh Mwanamilongo
1 Septemba 2023

Mashirika ya kutetea haki za binadamu likiwemo Human Rights Watch yametoa mwito wa uchunguzi wa haraka na kuchukuliwa hatua kwa viongozi wa jeshi waliohusika na mauwaji ya waandamanaji mjini Goma.

UN demands 'independent' probe into deaths at DR Congo rally
UN demands 'independent' probe into deaths at DR Congo rallyPicha: AFP

Shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu Human Rights Watch limelaani vikali mauwaji ya makumi ya waandamanaji mjini Goma. Thomas Fessy mtafiti mkuu wa Kongo kwenye shirika hilo amesema vikosi vya usalama nchini Kongo vilifyatua risasi kwenye umati wa watu kwa njia ya ukatili na isiyo halali.

Haki itendeke

Kwa upande wake, Mwanaharakati wa haki za binadamu Bienvenu Matumo kutoka vuguvugu la Kiraia la Pambania Mabadiliko, LUCHA nchini Kongo, amesema idadi ya watu waliouwawa imezidi hamsini huku akiilani utumiaji nguvu wa kuzidi kiasi.

''Ni mauwaji yaliofanywa na jeshi dhidi ya Wakristu waliopanga kuandamana kutaka wanajeshi (Umoja wa Mataifa ) wa Monusco waondoke. Tunachotaka ni haki itendeke. Wanajeshi wote waliohusika wakamatwe na kufunguliwa mashtaka.'', alisema Matumo.

Katika taarifa yake jana Alhamisi, msemaji wa serikali ya Kongo, Patrick Muyaya alitaja idadi ya waliofariki kuwa watu 43, huku 56 wakijeruhiwa na wengine 158 walikamatwa, akiwemo kiongozi wa waandamanaji hao. Serikali ilitangaza kuunga mkono uchunguzi ulioanzishwa na mwendesha mashataka wa jeshi na kuahidi kuwafikisha mahakamani wahusika.

Uchunguzi wa kimataifa ?

Umoja wa Mataifa siku ya Ijumaa ulidai uchunguzi "huru" baada ya makumi ya watu kuuawa katika msako mkali wa jeshi mjini Goma, jimboni Kivu ya KaskaziniPicha: Alain Wandimoyi/AFP

Awali gavana wa jimbo la Kivu ya Kaskazini Constant Ndima alitangaza kuwa idadi ya waliokufa ilikuwa ni watu 8 akiwemo polisi mmoja. Lakini maafisa wawili wa jeshi waliozungumza kwa sharti la kutotambulishwa, wamesema hospitali zilipokea malori kadhaa yaliobeba maiti tangu kutokea ukandamizaji huo na kusema idadi hiyo ni zaidi ya watu 48.

Mkuu wa shirika la kimataifa la Msalaba Mwekundu tawi la mjini Goma, alisema hospitali yake ilipokea idadi kubwa ya watu walio na majeraha mabaya ya visu na risasi baada ya makabiliano yaliyotokea. Wengine walikuwa wamekufa walipofikishwa hospitalani lakini hakuelezea idadi yao.

Chanzo kimoja cha Umoja wa Mataifa, kimesema wanachunguza madai ya vifo zaidi ya hamsini baada ya wanajeshi hao kuwazuia waandamanaji waliokuwa wamekusanyika kanisani kabla ya kuanza kwa maandamano kutaka kikosi cha wanajeshi wa Umoja wa mataifa Monusco kuondoka nchini Kongo.

 

Vyanzo : AFP na Reuters