Mashirika ya haki: Ubaguzi ukomeshwe Ufaransa
23 Julai 2021Faili lenye kurasa 220, lililojaa mifano ya kamatakamata ya polisi kwa misingi ya ubaguzi wa rangi wakati wa ukaguzi wa vitambulisho uliofanywa na polisi wa Ufaransa limewasilishwa kwa baraza la taifa, ambalo ni mamlaka ya juu zaidi katika suala la matumizi ya nguvu kwa mamlaka dhidi ya raia
Malalamiko hayo yaliwasilishwa na mashirika ya kutetea haki za binadamu ya Amnesty International, Human Rights Watch, taasisi ya Open Justice na mashirika mengine matatu ya wanaharakati yanayofanya kazi na vijana.
Hatua hiyo isiyotarajiwa inaorodhesha malalamiko ya muda mrefu ya matumizi mabaya ya mamlaka ya polisi katika kukagua vitambulisho hasa katika maeneo wanapoishi watu wasio wazungu.
Akizungumzia hatua ya kuwasilishwa kwa malalamiko hayo mkurugenzi wa shirika la Human rights watch mjini Paris Bi: Bénédicte Jeannerod; amesema hatua hiyo ni ya kihistoria na wanategemea sheria thabiti itakayoruhusu majaji wa mamlaka waagize serikali ichukue hatua stahiki ili kuondoa ubaguzi huu ambao umekuwepo kwa muda mrefu.
Wakosoaji wanasema ukaguzi wa namna hiyo ambao wakati mwingine hutumia nguvu na mara nyingi hufanywa mara kadhaa kwa mtu mmoja unaweza kuwaachia vijana doa katika maisha yao yote na kufanya mahusiano kati ya polisi na vijana kwenye maeneo husika kuwa mabaya zaidi.
Lengo la shauri ni kubadilisha sheria za kibaguzi
Asasi za kiraia nchini humo zinaituhumu polisi ya Ufaransa kwa kuwalenga watu weusi na wenye asili ya kiarabu katika kuchagua ni nani wa kumsimamisha na kumkagua. Shauri lililowasilishwa na asasi hizo linakusudia kupata mabadiliko makubwa kwenye jeshi la polisi ili kuhakikisha ubaguzi wa rangi wakati wa kuwakagua watu unakomeshwa.
Kati ya mambo mengine asasi hizo zinataka pia kuwepo na mafunzo kwa maafisa wa polisi na mfumo huru wa kutoa malalamiko ambapo kwa sasa yanachunguzwa na chombo cha ndani cha ndani cha polisi nchini humo.
Chombo hicho kinachojulikana kama IGPN kilirekodi malalamiko 72 ya matumizi ya nguvu ya polisi wakati wa kukagua vitambulisho kwa mwaka 2020 na malalamiko 38 ya matusi ya kibaguzi. Makundi ya haki za binadamu yanasema wengi wa walioathiriwa na vitendo hivyo mara nyingi huhofia kitakachowapata na hivyo hawaripoti malalamiko.