Maandamano yaitishwa dhidi ya ziara ya Mohammed bin Salman
26 Novemba 2018Rais wa Tunisia Beji Caid el Sebsi amesema kiongozi huyo wa Saudi atazuru taifa hilo kwa saa kadhaa kesho Jumanne ikiwa mojawapo ya ziara yake ya kimaeneo, bila kutoa maelezo zaidi kuhusiana na ratiba yake. Maandamano hayo yamepangwa kufanyika jioni ya leo katikati mwa mji wa Tunis na mji wa Sfax.
Saudi Arabia imekuwa ikipokea ukosoaji mkubwa wa kimataifa kufuatia mauaji ya Khashoggi mjini Istanbul tarehe 2 Oktoba mwaka huu. Kwenye barua kwa Ofisi ya Rais nchini Tunisa, muungano wa wanahabari nchini humo umesema kwamba ziara ya Mohammed Bin Salman inatishia usalama na Amani pamoja na ulimwengu, vile vile tishio kwa uhuru wa kujieleza. Aidha wanasema inakiuka kanuni ya mapinduzi.
Uchunguzi wa kutafuta mabaki ya mwili wa Khashoggi
Hayo yakijiri, maafisa wa polisi wa Uturuki pamoja na mbwa wa kunusa wamefanya ukaguzi katika majengo mawili ya kifahari Magharibikaskazini mwa Uturuki leo, ikiwa mwendelezo wa uchunguzi wa mauaji ya Jamal Khashoggi. Maafisa wanaoendeleza uchunguzi huo wamesema kwamba kisima kilichoko kwenye mojawapo ya majengo hayo ndiho kilichokuwa kikilengwa, huku taarifa katika vyombo vya habari vya Uturuki vikisema kuwa walikuwa wakitafuta mabaki ya mwili wake.
Gazeti la Hurriyet limesema moja wapo ya majengo hayo mawili ya kifahari yanamilikiwa na mfanyabiashara mmoja wa Saudi Arabia lakini hawakumtaja jina. Gavana wa eneo la Yalova Mummaer Erol amesema kwamba tangazo kuhusiana na msako unaoendelea litatolewa na mkuu wa mashtaka anayeongoza uchunguzi wa taifa la Uturuki kuhusiana na mauaji hayo.
Uturuki imesisitiza kwamba maagizo ya kuuawa kwa Khashoggi yalitolewa na mmoja wa wakuu wa serikali ya Saudi,lakini sio Mohammed bin Salman. Salman alianza ziara yake kufuatia ombi la baba yake Mfalme Salman, ikiwa ni kulingana na Idara ya Habari ya Saudi,ambayo ilisema atazuru mataifa ya Kiarabu. Mrithi huyo wa Ufalme atawasili mjini Cairo Misri kufanya mazungumzo na Rais Abdel Fatah al-Sisi. Anatarajiwa kuhudhuria mkutano wa G20 nchini Argentina wiki ijayo.
Mwandishi: Sophia Chinyezi/AFPE/APE
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman