1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIsrael

Netanyahu asema huenda vita vikachukua muda mrefu

24 Oktoba 2023

Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ameonya hii leo juu ya uwezekano wa vita vya muda mrefu dhidi ya kundi la wanamgambo la Hamas akisema kundi hilo ni lazima litokomezwe.

Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesisitiza kwamba kundi la Hamas linafanya uhalifu mkubwa wa kivita sio tu dhidi ya Israel bali pia kwa raia wao
Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesisitiza kwamba kundi la Hamas linafanya uhalifu mkubwa wa kivita sio tu dhidi ya Israel bali pia kwa raia waoPicha: Jacquelyn Martin/Pool via REUTERS

Waziri mkuu Netanyahu amelituhumu kundi la Hamas kwa mauaji, ubakaji na uhalifu dhidi ya raia na kuahidi kuchukua hatua za kulizuia. Netanyahu amesema hayo wakati vita vyake dhidi ya Hamas vikifikia siku ya 18 huku kukiripotiwa vifo vya zaidi ya Wapalestina 700 kufuatia mashambulizi ya Israel ya usiku wa kuamkia leo. 

Soma zaidi:Hamas: Vifo vyapindukia 5,000 Gaza 

Waziri mkuu Benjamin Netanyahu ametoa matamshi hayo alipozungumza na rais wa Ufaransa Emmanuel Macron aliyekwenda Israel kuonyesha mshikamano na taifa hilo. Amesisitiza kwamba Hamas wanahusika na uhalifu dhidi ya raia, lakini akiahidi kufanya kila linalowezekana kuwazuia na kuongeza kasi ya vita hivyo. Netanyahu akaongeza kuwa kwa ujumla, Hamas inafanya uhalifu wa kivita si tu dhidi ya Israel bali pia dhidi ya raia wao.

"Kwa hiyo tunafanya kila liwezekanalo kuliteketeza Hamas huko Gaza. Tutavunjavunja mfumo wake wa kisiasa. Tutafanya kila juhudi kuwapata mateka wanaoshikiliwa. Na tutafanya kila juhudi kuwalinda raia wa Palestina dhidi ya Hamas."

Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu akipeana mkono na rais wa Ufaransa Emmanuel Macron alipozuru Israel kuonyesha mshikamanoPicha: CHRISTOPHE ENA/AFP

Macron atoa wito wa kuungana kupambana na makundi ya kigaidi.

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron kwa upande wake amependekeza kuchukuliwa hatua za pamoja na zitakazoratibiwa kimataifa dhidi ya Hamas. Amenukuliwa akiwaomba washirika wao wa kimataifa kuunda muungano wa kikanda na kimataifa kupambana na makundi kama hayo yanayoibua kitisho dhidi yao. Macron anakuwa kiongozi wa kwanza wa mataifa ya magharibi kukutana na waziri mkuu wa Israel na rais wa Palestina.

Macron amesema muungano unaokabiliana na kundi la wanamgambo linalojiita Dola la Kiislamu, IS nchini Syria na Iraq unaweza kupanua operesheni zake na kulihusisha pia kundi la Hamas. Hata hivyo hakufafanua zaidi juu ya namna muungano huo unaoongozwa na Marekani, ambao Israel sio mwanachama unavyoweza kufanya hivyo.

Huko Gaza, wizara ya afya imesema zaidi ya Wapalestina 700 wameuawa katika mashambulizi ya Israel ya usiku kuamkia leo, ikiwa ni idadi ya juu kabisa kushuhudiwa katika kipindi cha masaa 24 tangu Israel ilipoanzisha kampeni yake dhidi ya Hamas. Israel kwa upande wake imesema imewaua makumi ya wanamgambo wa Hamas katika mashambulizi hayo ya jana usiku.

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Annalena Baerbock amerudia tena kutoa wito wa kusitishwa mapigano na kuruhusu kupitishwa misaadaPicha: Thomas Koehler/photothek/IMAGO

Umoja wa Mataifa watahadharisha juu ya janga la kibinaadamu, Gaza

Taarifa kutoka New York zimesema waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Annalena Baerbock amesisitiza kwa kutoa wito wa kusimamishwa mapigano ili kuruhusu kupitishwa kwa misaada ya kiutu huko Ukanda wa Gaza. Amesema hayo kabla ya mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Baerbock anatoa wito huo huku shirika la afya ulimwenguni, WHO likirudia kuonya tena juu ya hali tete katika Ukanda wa Gaza , likiangazia zaidi upungufu mkubwa wa maji. Mkurugenzi wa kikanda wa WHO Rick Brennan amekadiria kwamba kila mtu amebakiwa na lita tatu tu za maji, tofauti na mahitaji ya kawaida ya lita 15 kwa ajili ya kunywa, kupika na usafi. Amesema ni suala la muda tu, eneo hilo litakabiliwa na mlipuko wa maradhi ya kuhara, ngozi na upumuaji.

Huku hayo yakiendelea, mwanamke mmoja wa miaka 85 raia wa Israel aliyeachiliwa na Hamas amesema alipitia machungu makali alipokuwa akishikiliwa lakini anasema alihudumiwa vizuri wakati alipokuwa akizuiwa huko Gaza. Mwanamke huyo Yocheved lifshitz amesema mtu mwenye silaha alikuwa akimpiga wakiwa njiani, na kuongeza kuwa ingawa hawakumvunja mbavu, lakini walimuumiza sana. Hamas bado inamshikilia mume wake na mateka wengine 200.

Soma pia: UN: Mzozo wa Israel na Hamas umefikia hatua mbaya