Mashirika ya kimataifa yaruhusiwa kuzuru jimbo la Rakhine
28 Septemba 2017Umoja wa Mataifa umekuwa ukitaka kuzuru eneo hilo tangu mashirika ya kiutu yalipolazimika kuondoka katika jimbo la Rakhine wakati Myanmar ilipoanzisha operesheni ya kijeshi dhidi ya jamii hiyo ya wa Rohingya ambao ni waislamu, mwishoni mwa mwezi Agosti na kusababisha mamia kwa maelfu kukimbilia katika nchi jirani ya Bangladesh.
"Kutakuwa na safari iliyoandaliwa na serikali kuzuru jimbo la Rakhine" alisema msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric na kuongeza kuwa ana matumaini kuwa ni hatua moja wapo katika kuelekea kupata uhuru na urahisi zaidi wa kuzuru jimbo hilo.
Dujarric ameongeza kuwa mkuu wa mashirika ya Umoja wa Mataifa atakuwemo katika ziara hiyo.
Umoja wa Mataifa umeandaa mpango wa dharura kwa ajili ya huduma ya chakula kwa wakimbizi wa Rohingya 700,000.
Afisa mtendaji mkuu msaidizi wa shirika la mpango wa chakula duniani Dipayan Bhattacharyya amaesema hii leo kuwa mashirika yote ya Umoja wa Mataifa yameandaa mpango mpya kwa ajili ya wakimbizi 700,000 wa jamii ya Rohingya.
Mtendaji Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya wakimbizi Fillippo Grandi amesema kwa wale ambao tayari wamekimbilia Bangladesh kurejea kwao kutachukua muda iwapo itatokea na iwapo vurugu zitasimama.
Wahoringya wanakabiliwa na dhiki
Grandi amesema katika majukumu yake, hajawahi kuona watu wenye dhiki kama wakimbizi hawa warohingya.
Jeshi la Myanmar ambalo limekuwa likishutumiwa kuzuia upatikanaji habari kuhusina na operesheni inayoendelea katika mji wa Maungdaw magharibi mwa nchi hiyo hapo jana iliandaa ziara ya vyombo vya habari katika kijiji cha Baw Kyaw ambayo hata hivyo taarifa za hivi punde zinasema zira hiyo imefutwa..
Makaburi makubwa yaliyozikwa miili ya wanavijiji 45 wa jamii ya Kihindu yaligundulika mapema wiki hii na jeshi la nchini hiyo linawashutumu wanamgambo kutoka jamii hiyo ya warohingya kwa kuhusika na mauaji hayo.
Hata hivyo kikundi cha uwokozi cha wanamgambo wa Rohingya kimekanusha wanamgambo wake kuhusika na mauaji hayo pamoja na vitendo vya udhalilishaji kingono au kuwasajli kwa nguvu watu katika jeshi hilo.
Mifupa na miili ya watu waliouawa ilikutwa katika majani katika eneo la Ye Baw Kyaw huku watu wa jamii ya kihindu waliokimbia eneo hilo wakilieleza shirika la habari la AFP kuwa washambuliaji waliokuwa wamefunika sura zao walivamia eneo hilo na kuwakatakata baadhi ya watu kwa mapanga na baadaye kuwafukia.
Jeshi la Myanmar limekuwa likijaribu kudhibiti taarifa kuhusiana na mgogoro huo ikiwa ni pamoja na kuzuia vyombo vya habari kuzuru eneo lenye mgogoro huku likitoa taarifa za mara kwa mara likiwashutumu wanamgambo wa Rohingya kwa kuhusika na umwagaji damu.
Taarifa za serikali pamoja na jeshi zimekuwa pia zikijaribu kuelezea mateso wanayokabiliwa nayo watu wa jamiii nyingine nchini humo kama vile wabudha walioko katika jimbo la Rakhine na wahindu ambao wameondolewa katika eneo ambalo limekumbwa na machafuko.
Mwandishi: Isaac Gamba/rtre/afpe
Mhariri : Gakuba Daniel