1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Gaza: Mashirika ya misaada yatahadharisha juu ya baa la njaa

29 Februari 2024

Wapatanishi waeleza tamaa ya kufikiwa makubaliano ya kusitisha vita kati ya Israel na Hamas huku mashirika ya misaada yakitoa tahadhari ya kuzuka baa la njaa kaskazini mwa Ukanda wa Gaza..

Wapalestina wasubiri msaada wa chakula katika mji wa Rafah wa kusini mwa Ukanda wa Gaza.
Wapalestina wasubiri msaada wa chakula katika mji wa Rafah wa kusini mwa Ukanda wa Gaza.Picha: Abed Zagout/Anadolu/picture alliance

Wapatanishi kutoka Misri,Qatar na Marekani wanapendekeza kusitishwa vita hivyo kwa muda wa wiki sita.

Wanatumai kwamba makubaliano hayo yanaweza kuanza mwanzoni mwa mwezi mtukufu kwa Waislamu wa Ramadhan ambao unatarajiwa kuanza Machi 10 au 11, kulingana na kuandama kwa mwezi kwa mujibu wa kalenda ya Kiislamu.

Soma Pia: Israel na Hamas wakaribia kufikia mkataba wa kusitisha vita

Mengineyo katika mapendekezo hayo ni pamoja na kuachiwa kwa baadhi ya mateka wa Israel wanaoshikiliwa huko Gaza ili kufungua njia ya kubadilishana na mamia ya wafungwa wa Kipalestina wanaoshikiliwa na Israel.

Mratibu wa Shirika la Misaada la Marekani (USAID) Samantha PowerPicha: Jose Cabezas/REUTERS

Ama kulingana na tahadhari ya kuzuka baa la njaa katika eneo la kaskazini mwa Gaza iliyotolewa na mashirika ya misaada, mratibu wa shirika la misaada la Marekani (USAID) Samantha Power, amesema ni vyema kamaIsrael itafungua vivuko zaidi ili misaada inayohitajika sana iweze kuingia kwa wingi na kwa kasi.

Soma Pia:Haniyeh: Tuko tayari kwa mazungumzo, lakini pia kuendeleza mapigano

Naibu mkurugenzi wa Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) Carl Skau, amesema mashirika ya misaada yameshindwa kupeleka misaada kaskazini mwa Gaza kwa zaidi ya mwezi mmoja sasa na ameongeza kusema kuwa iwapo hali hiyo haitabadilika basi eneo hilo litakumbwa na njaa kubwa.

Hata hivyo maafisa wa Israel wamekanusha kauli hiyo ya WFP ambapo jeshi la Israel limesema malori 50 yaliyobeba misaada ya kibinadamu yaliingia kaskazini mwa Gaza katika siku chache zilizopita.

Vita hivyo vilichochewa na mashambulio ya Hamas mnamo Oktoba 7 kusini mwa Israel ambapo watu wapatao 1,160, wengi wao wakiwa raia, waliuawa.

Soma Pia:Hamas iko tayari kwa mazungumzo juu ya kuachiliwa kwa mateka

Wanamgambo wa Hamas pia waliwachukua mateka watu wapatao 250. Mpaka sasa mateka 130 bado wameshikiliwa katika Ukanda wa Gaza. Serikali ya Israel imesema mateka 31 wanadhaniwa kuwa wameuawa.

Ujerumani, Marekani, Umoja wa Ulaya na mataifa mengine yameliorodhesha kundi la Hamas kama kundi la Kigaidi.

Familia za mateka wa Israel wanaoshikiliwa na Hamas katika Ukanda wa Gaza zaandamana kudai wapendwa wao waachiliwe huru.Picha: Tsafrir Abayov/AP Photo/picture alliance

Wakati huo huo familia za mateka wa Israel wanaoshikiliwa huko Gaza na wafuasi wao wameanza matembezi ya siku nne kutoka kusini mwa Israel kuelekea katika mji wa Jerusalem wakidai wapendwa wao waachiwe huru.

Vyanzo: AFP/AP