Mashirika ya ndege ya kimataifa yaongeza safari Tanzania
2 Septemba 2020Katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kilimanjaro KIA uliopo kaskazini mwa Tanzania , ndege ya shirika la ndege la Ethiopia Dream liner iliwasili ikiwa na abiria 18 kutoka mataifa mbali mbali yakiwepo ya ulaya na Marekani. Baadhi ya abiria wa kigeni kutoka mataifa hayo wanaeleza kuwa wamekuja Tanzania kwa sababu ya masuala mbali mbali kama vile kufanya utafiti na kutembelea maeneo ya vivutio vya utalii. Mason Kaima ni raia kutoka nchini Marekani na anasema, "nafanya kuwasaidia vijana ambao hawakufanikiwa kumaliza elimu ya juu, na pia ninafanya miradi ya kilimo na kusaidia wanawake. Nitakuwa hapa mpaka mwezi wa kwanza mwaka kesho na hii ni mara yangu ya kwanza kufika Afrika.”
Ndege hiyo ya Ethiopia kwa sasa itakuwa inatua Tanzania mara 14 kwa juma kutoka safari tatu za mwanzo, shirika la ndege la Qatar limeongeza safari 10 na sasa itakuwa inatua katika viwanja vya Tanzania mara 12 kutoka safari mbili za mwanzo, huku shirika la ndege la Uholanzi la KLM ndege zake zitatua katika viwanja vya Tanzania mara nne kwa juma.
Shirika la ndege la Rwanda Rwanda Air nalo limetangaza kuongeza safari zake nchini Tanzania mara nne kutoka mara mbili kwa juma, huku serikali ya Tanzania ikisema kuongezeka kwa safari hizo kunaifanya Tanzania kupiga hatua katika kufufua tena matumaini ya biashara ya utalii iliyoporomoka pabubwa kutokana na janga la Corona kulingana na mkuu wa wilaya ya Kilimanjaro Anne Mghwira.
Tanzania ilikuwa nchi ya kwanza katika mataifa ya Afrika mashariki kufungua anga zake na kuruhusu wageni kutoka maeneo mbali mbali kuingia nchini humo baada ya kuzifunga kutokana na janga la corona.
Veronica Natalis DW Kilimanjaro.