1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mashirika ya ndege yawazuia wanaharakati wa Palestina kuruka

8 Julai 2011

Mashirika ya ndege ya Ulaya yamewazuia mamia ya wanaharakati wanaouinga mkono Palestina kusafiri kupitia Israel kushiriki kampeni ya "Karibu Palestina" inayodhamiria kukiuka vizuizi vya Israel kwa Ukanda wa Gaza.

Mwanaharakati wa Kipalestina akishikiliwa na polisi katika uwanja wa ndege wa Ben-Guiron
Mwanaharakati wa Kipalestina akishikiliwa na polisi katika uwanja wa ndege wa Ben-GuironPicha: picture alliance/dpa

Kiasi ya wanaharakati 200 hawajaweza hadi sasa kuondoka kwenye viwanja vya ndege vya Ufaransa, Ujerumani na Uswisi, na tayari mamlaka nchini Israel imeshaanza kuwarudisha wale wachache waliowahi kupenya, kusafiri na kutua kwenye uwanja wa ndege wa nchi hiyo wa Ben-Guiron.

Ingawa msemaji wa jeshi la polisi wa Israel, Micky Rosenfeld, ametumia lugha ya kidiplomasia kusema nchi yake inawaruhusu kuingia Israel watu wa amani na wasio wachokozi tu, lakini Waziri wake wa Usalama wa Ndani, Yitzhak Aharonovic, amefika umbali wa kuwafananisha wanaharakati hao na makundi ya itikadi kali na wahuni, akiapa kwamba hawataikanyaga ardhi ya Israel.

"Hatowasili hapa. Tutahakikisha hawaingii nchini mwetu. Amri imeshatolewa, na atakayeingia na kutambuliwa atarudishwa haraka." Amesema Aharonovic.

Kundi hili la wanaharakati linataka kuingia Ukingo wa Magharibi kupitia uwanja wa ndege wa Ben-Guiron ulio karibu na mji mkuu wa Israel, Tel-Aviv, kwa kuwa Palestina haina uwanja wake wa ndege.

Waratibu wa vuguvugu la "Karibu Palestina" wanasema kiasi ya wanaharakati 800 walitarajiwa kuingia Palestina katika kampeni ya amani ya kuzitembelea familia za Kipalestina.

Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin NetanyahuPicha: picture alliance / dpa

Uamuzi wao huu unafuatia hatua za serikali ya Ugiriki kuzuia msafara wa meli za misaada kutoka Athens kung'oa nanga kuelekea Gaza, kwa kile kinachosemekana ni kutii shinikizo la Israel.

Kwa mujibu wa gazeti kubwa nchini Israel, Yedioth Ahronoth, serikali ya Israel imeyapa mashirika ya ndege ya Ulaya orodha ya wanaharakati 342, ambao watarudishwa kama watatua uwanja wa ndege wa Ben-Gurion na kwamba mashirika hayo yatabeba gharama za kurudishwa huko.

Akitetea uamuzi huu, Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, amesema ni kwa ajili ya kulinda usalama wa nchi yake kwa kuwa kuingia kwa wanaharakati hao kwenye ardhi yake kutachochea machafuko kutoka kwa Wapalestina.

Mmoja wa wanaharakati waliozuiliwa kupanda ndege kutokea uwanja wa ndege wa Berlin, Ujerumani, Cynthia Beat, amesema ameshtushwa sana kuwekwa kwenye orodha ya watu wasioruhusiwa kupanda ndege, bila ya ushahidi wa kufanya kosa lolote.

Muandaaji mmoja wa vuguvugu la "Karibu Palestina", Sophia Deeg, amesema kwamba dhamira ya kampeni yao ni kupeleka ujumbe wa wazi wa Israel.

"Msafiri huwa anamuambia afisa wa uhamiaji: 'Tunawatembelea marafiki zetu wa Kipalestina. Hatuna njia nyengine ya kuwafikia marafiki zetu bila ya kupitia kwenye mipaka ya Israel kwa kuwa mumeizingira Palestina.'" Amesema Deeg.

Wanawake wawili wa Kimarekani ambao waliruka na ndege ya usiku wa jana, walikamatwa walipotua tu nchini Israel na kurudishwa walikotoka, kwa kile msemaji wa polisi wa Israel, Micky Rosenfeld, alichokiita kuwa ni "matatizo ya kiusalama."

Polisi pia imewakamata Waisraili sita ambao walikuwa wakipinga hatua hizi za serikali yao. Mmoja ya Waisraili hao alipiga mayowe kwa Kiarabu "Palsetina Huru", huku akiburuzwa na polisi kutolewa nje ya uwanja.

Tayari wanaharakati wengine 20 waliongia uwanja wa ndege wa Ben-Gurion wakitokea Uswisi, wako mikononi mwa maafisa wa usalama wa Israel na inatarajiwa watarudishwa makwao muda mchache ujao.

Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters
Mhariri: Othman Miraji

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi
Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW