Mashirika ya Umoja wa mataifa yapeleka misaada Afghanistan
24 Juni 2022Tetemeko hilo limesababisha vifo vya watu 1,036 na idadi hiyo inayotarajiwa kuongezeka. Kulingana na maafisa wa Afghanistan wamesema siku ya Ijumaa.
Shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia wakimbizi (UNHCR), limepeleka vifaa vya makazi na kaya, ikiwemo mahema 600 na taa 1,200 zinazotumia umeme wa jua, ili kuwasaidia watu takribani 4,200 walionusurika. Kulingana na Msemaji wa UNHCR, Shabia Mantoo, aliuambia mkutano huko mjini Geneva.
UNHCR imepeleka wafanyakazi ambao watapanga makazi ya watu ambao wamepoteza makazi yao na kuanzisha vituo vya usambazaji wa msaada kutoka mji mkuu wa Afghnanistan, Kabul. Ameongezea kuwa, kuna hatari kubwa ya kuenea kwa magonjwa ya kuambukiza.
Shirika la Afya Duniani (WHO), imeonya kuwa, janga hilo linaweza kuzidisha mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu, kwani tayari umeenea nchi nzima. Takriban watu 500,000 walionekana na dalili za ugonjwa huo mwezi Mei, alisema Dokta Dapeng Luo, mwakilishi wa WHO nchini Afghanistan.
Maelfu ya nyumba zimeharibiwa na tetemeko la ardhi, kulingana na mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa, linaloshughulikia masuala ya watoto (UNICEF) nchini Afghanistan, aliuambia mkutano huo. "Watoto na vijana wapo kwenye hatari ya kutengana na familia, kuathirika kihisia na kisaikolojia, unyanyasaji na ukatili,'' alifafanua Dokta Luo.
Tetemeko hilo la ardhi lililokuwa na ukubwa wa 6.1 katika kipimo cha Richta, limelotokea kwenye majimbo ya Paktika na Khost, karibu Kilomita 160 (maili 100) kusini mashariki mwa Kabul, karibu na mpaka wa Pakistan.
Mawasiliano duni na ukosefu wa barabara zenye viwango duni, ni vikwazo kwa usambazaji wa misaada katika nchi hiyo, kwani imekuwa ikikabiliwa na mgogoro tangu Taliban ichukue madaraka Agosti iliyopita.
Mnamo 2015, tetemeko la ardhi lilitokea maeneo ya kaskazini-mashariki mwa Afghanistan na kusababisha mamia ya watu kupoteza maisha.
(Reuters)