1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mashirika yasiokuwa ya kiserikali yapinga teknologia mpya ya GMO

Mwakideu, Alex16 Mei 2008

Mwanaharakati wa India Vandana Shiva amesema utafiti kuhusu teknologia ya GMO inayomaanisha kuboresha mimea na mbegu kwasababu ya mazao makubwa inaingizwa kwa lazima duniani

Mmoja wa wanahakati wa kulinda mazingira Vandana Shiva kutoka India ambaye amehudhuria kikao cha Umoja wa Mataifa mjini Bonn UjerumaniPicha: picture-alliance/ dpa

Wakati dunia inakabiliwa na upungufu wa chakula, imebainika leo kwamba upungufu huo huenda ukaongezeka zaidi.


Takribani nchi 200 zinatarajiwa kukutana kuanzia wiki ijao katika kikao cha Umoja wa Mataifa kilichoandaliwa hapa mjini Bonn Ujerumani kwa minajili ya kujadili maswala ya kuokoa bayo anuai. Tayari mkutano huo umepokea upinzani mkali kutoka kwa mashirika yasiokuwa ya kiserikali.


Kikao hicho kimechukua mwelekeo mwengine leo baada ya mashirika mbali mbali ulimwenguni yanayopinga teknologia mpya ya kutumia sayansi kuboresha mimea kutoa misimamo wake.


Katika taarifa kwa vyombo vya habari mashirika hayo yamesema teknologia hiyo mpya inayoifanya mimea izalishe zaidi inaingizwa kwa lazima bila kujali maafa ya siku za usoni.


Mamadou Goita ambaye ni mwanachama wa muungano wa kulinda asili ya genetiki ya Afrika yaani Coalition for the Protection of African Genetic Heritage amesema teknologia hiyo inaongeza matatizo duniani "hii inamaanisha kuleta tatizo lengine tena katika bara hili kando na lile tunalokumbana nalo kwa sasa kwahivyo hivi vita vinahusu ubeberu ambao hawa watu wanajaribu kutuletea mpango wa chakula sasa upo mikononi mwa shirika la biashara ulimwenguni na mashirika mengine na mambo hayatakikani kuwa hivyo" Mamadou amesema.


Mwanasayansi Vandana Shiva ambaye pia ni mwanaharakati wa kupigania uwepo wa mazingira bora ameunga mkono maneno hayo akisema jaribio la kutengeneza mbegu za kutoa mazao makubwa zaidi zinazojulikana kwa lugha ya kitaalamu kama GMO, limegonga mwamba "Halikufaulu kidemocrasia, kwasababu hakuna nchi yoyote ambapo teknologia ya GMO imeingizwa kupitia maoni ya wananchi bali inaingizwa kwa kufisidi maagenti kadhaa wa serikali. Jaribio hilo halikufaulu pia kwasababu ahadi zilizotolewa hazijaafikiwa. Ahadi zilikuwa chakula zaidi, ahadi zilikuwa mazingira bora zaidi lakini kile tunachoona katika miaka yote ishirini ya majaribio na mauzo ya GMO ni nchi nne na mbegu nne za maragwe, mahindi, kanola na pamba biashara mbili na kampuni moja inayoongoza asilimia 95 ya mbegu za GMO"


Amesema teknologia hiyo inapunguza uwezo wa kuzalisha vyakula vingi tofauti na isitoshe inatishia afya ya binadamu na kuongeza matatizo duniani.


Waziri wa mazingira nchini Ujerumani Sigmar Gabriel anatarajiwa kufungua kikao cha wiki ijayo na kuhutubia katika siku tatu za mwisho za kikao hicho kitakachohudhuriwa pia na maafisa wakuu wa nchi 191 akiwemo kansela wa Ujerumani Angela Markel.


Wajumbe watajaribu kusonga mbele na mazungumzo ya kutunga sheria kabla ya mwaka wa 2010. Sheria hizo zitahusu matumizi ya rasilimali ya genetiki na ugavi wa faida zake; mambo ambayo yana umuhimu zaidi kwa nchi zinazoendelea, kampuni za dawa na teknologia ya bayo.


Wanatarajiwa pia kujadili njia za kuboresha na kulinda maeneo yanayohifadhiwa kwa minajili ya kubakisha asili ya mazingira.


Kulindwa kwa bahari na misitu pia kutatiliwa maanani. Kikao hicho kina lengo la kulinda angalau asilimia 10 ya viumbe na mazingira.


Wataalamu wanasema asilimia 80 ya bayo anuai inapatikana katika misitu ya nchi za joto lakini kila dakika 20 hekari hamsini ya misitu hiyo inapotea.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW