1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Chama tawala chashindwa uchaguzi mkuu Botswana

Angela Mdungu
1 Novemba 2024

Chama tawala cha Botswana BDP cha Rais Mokgweetsi Masisi kimeshindwa katika uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 30. Ushindi huo unahitimisha miaka 58 ya utawala wa chama hicho madarakani.

Masisi amekiri kushindwa katika uchaguzi wa Oktoba 20, 2024
Rais wa Botswana Mokgweetsi Eric MasisiPicha: Dominika Zarzycka/NurPhoto/picture alliance

Tayari Rais Mokgweetsi Masisi amekiri kushindwa kwenye kinyang'anyiro hicho baada ya matokeo ya awali kuonesha kuwa chama chake kimepoteza wingi wa viti bungeni.

Masisi amesema ameshazungumza na kiongozi wa chama cha upinzani cha mrengo wa kushoto cha UDC cha mgombea Duma Boko ili kupanga namna ya kukabidhi madaraka.

Ushindi wa upinzani nchini humo ambao haukutarajiwa ni pigo kubwa chama tawala na Masisi aliyeingia madarakani mwaka 2018.  Chama chake kimekuwa madarakani tangu Botswana ilipopata uhuru kutoka kwa Uingereza mnamo mwaka 1966.

Soma zaidi: Botswana yafanya uchaguzi mkuu

Zaidi ya watu milioni moja walijiandikisha kupiga kura katika uchaguzi huo kati ya raia milioni 2.6 wa taifa hilo. Chama kilichoshinda cha UDC kilianzishwa na Duma Boko mnamo mwaka 2012 kwa nia ya kuunganisha makundi ya upinzani dhidi ya chama tawala.

Hii ni mara ya tatu kwa Boko ambaye pia ni mwanasheria kuwania Urais. Aidha baada ya matokeo ya awali kupitia ukurasa wake wa Facebook kiongozi huyo wa upinzani ameandika "mabadiliko yamewadia". Kando ya kupata wingi wa viti bungeni chama cha Boko kimepata pia ushindi mkubwa katika uchaguzi tofauti wa serikali za mitaa.

Wingi wa viti vya bunge umeupa ushindi upinzani

Kulingana na televisheni ya taifa, chama cha UDC kimeshinda viti 26 kati ya 61 vinavyowaniwa wakati chama tawala cha BDP kikiwa na viti viwili pekee. Matokeo hayo yametengeneza njia kwa mgombea wa UDC kushinda urais. Kwa mujibu wa katiba ya nchi hiyo,  wabunge ndiyo wanaomchagua Rais.

Mgombea urais wa Botswana kupitia chama cha UDC Duma BokoPicha: Monirul Bhuiyan/AFP

Japokuwa matokeo ya mwisho hayajatangazwa rasmi na tume ya uchaguzi ya taifa hilo, matokeo hayo ya awali yanamaanisha kuwa Chama cha Masisi hakiwezi tena kupata viti vya kutosha kuunda serikali.

Licha ya ushindi, Boko atakabiliwa na changamoto nyingi zinazowakabili raia ukiwemo ukosefu wa ajira ulioongezeka kwa asilimia 27 mwaka huu. Nchi hiyo inakabiliwa pia na kuporomoka kwa uchumi ambako kwa sehemu moja kumesababishwa na kushuka kwa mauzo ya almasi ambayo inategemewa kwa kiasi kikubwa kuiingizia kipato Botswana.

Kando ya masuala hayo serikali mpya itakayoongoza nchi hiyo itatazamiwa kupambana na rushwa, upendeleo na usimamizi mbovu wa mamlaka za serikali iliyopita huku tofauti kati ya walionacho na wasio nacho nchini humo ikiwa ni kubwa zaidi duniani, kwa mujibu wa benki ya dunia.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW