1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Masuala ya Afrika yaliyoandikwa katika magazeti ya Ujerumani

Daniel Gakuba
21 Aprili 2023

Wiki hii wahariri wa magazeti ya Ujerumani wameangazia matukio yaliyojiri barani Afrika mnamo wiki hii inayomalizika, yakiwemo hali ya wahamiaji wa Kiafrika nchini Tunisia na utawala wa kiimla Eswatini.

Deutschland Berlin wird Regierungssitz
Picha: Andreas Altwein/dpa/picture alliance

Tunaanza na gazeti la Die Tageszeitung lililoandika juu ya madhila ya wahamiaji kutoka nchi za kusini mwa jangwa la Sahara wanaoishi nchini Tunisia, chini ya kichwa cha habari kisemacho, Tunisia yawafukuzia baharini wafamiaji.

Mwandishi wa gazeti hilo anasimulia juu ya operesheni ya polisi dhidi ya kambi ya mahema iliyojengwa na wahamiaji hao mbele ya ofisi ya shirika la Umoja wa Mataifa kwa ajili ya wakimbizi, UNHCR mjini Tunis, na kuwatawanya waliokuwa katika kambi hiyo.

Mgogoro huo ulianza baada ya kauli ya Rais Kais Saied wa Tunisia tarehe 21 Februari, ambapo alidai Wafrika weusi wanaohamia nchini mwake wana njama ya kuubadilisha utambulisho wa nchi hiyo kama taifa la kiarabu na kiislamu.

Wengi wa wahamiaji hao weusi kutoka Afrika Magharibi na ya Kati wanaokadiriwa kuwa 50,000 nchini Tunisia, wanafanya kazi za malipo ya chini zilizoachwa na vijana wa Tunisia wanaliohamia kwa wingi barani Ulaya.

Wahamiaji wa Kiafrika wanakabiliwa na ukndamizaji nchini TuniiaPicha: Hasan Mrad//IMAGESLIVE via

Ripoti ya gazeti hili inasema japo hali imetulia kidogo, hatua ya serikali ya Tunisia kuwashinikiza wahamiaji hao kulipa faini kubwa iwapo wamesalia zaidi ya miezi mitatu inayoruhusiwa, inawafanya kukimbilia katika maboti wakijaribu kwenda Italia kupitia Bahari ya Mediterania.

Mmiliki wa mgahawa mmoja mjini Tunis ambaye alikuwa na wafanyakazi wahamiaji, alisema serikali ya Tunisia inawatumia Waafrika hao kutoka Kusini kwa Sahara kama kisingizio kwa matatizo ya kiuchumi yanayoikumba nchi hiyo ya Afrika Kaskazini.

Maslahi ya Ujerumani kiusalama katika Ukanda wa Sahel

''Kutoka Mali na kuhamia Niger'' ni kichwa cha habari cha ripoti ya gazeti la Berliner Zeitung, inayoangazia sera ya Ujerumani kuhusu Ukanda wa Sahel. Ripoti hiyo inaitazama ziara ya waziri wa ulinzi wa Ujerumani Boris Pistorius na wa ushirikiano wa  kimaendeleo Svenja Schulze nchini Niger.

Inamnukuu waziri wa ulinzi Pistorius akisema Ujerumani inayo maslahi makubwa katika usalama wa Sahel, na kwa hivyo kuwaondoa wanajeshi wa wake kutoka Mali ni zoezi litakalofanyika taratibu na kwa mpangilio, na kuhitimishwa Mei mwaka 2024.

Mawaziri hao ambao waliizuru pia Mali, walisema Niger ndio makao makuu ya baadaye ya ushirikiano wa kijeshi kati ya Ujerumani na ukanda wa Sahel. Ziara yao hiyo ilikwenda sambamba na tukio la kurefushwa kwa mara ya mwisho kwa muda wa vikosi vya Ujerumani katika Ujumbe wa amani wa Umoja wa Mataifa nchini Mali-MINUSMA, na kuanzishwa kwa ngwe mpya ya ushiriki wa vikosi hivyo vya Ujerumani katika ujumbe wa Umoja wa Ulaya wa ushirikiano wa kijeshi na Niger.

Waziri wa ulinzi wa Ujerumani, Boris Pistorius (kushoto) na mwenzake wa Niger Alkassoum Indatou mjini NiameyPicha: Michael Kappeler/dpa/picture alliance

Uamuzi wa Ujerumani kuwaondoa wanajeshi wake 1100 kutoka katika ujumbe wa MONUSMA ulifuatia mikwaruzano ya mara kwa mara na utawala wa kijeshi wa Mali, ambao unaonekana kuegemea zaidi upande wa Urusi.

Miaka 50 ya utawala wa kiimla nchini Eswatini

Die Tagesspiegel limezimulika siasa za Eswatini, taifa dogo la kusini mwa Afrika linalotawaliwa na mfalme ambalo zamani lilijulikana kama Swaziland. Kichwa cha habari cha ripoti yake kinasema, ''Miaka 50 ya ugaidi wa kiserikali nchini Eswatini,'' na kufuatia na swali, ni lini mfalme atawapa uhuru watu wake? Kisha, ripoti hiyo inasema Aprili imetimia miaka 50 tangu aliyekuwa aliyekuwa mfalme wakati huo, Sobhuza kupiga marufuku vyama vya upinzani mwezi Aprili mwaka 1973. Kuanzia wakati huo katiba ilifutwa, na amri ya mfalme ikawaweka katika kundi la magaidi, watu wote watakaoonyesha hisia za upinzani.

Leo hii taifa hilo linatawaliwa na Mfalme Mswati lll ambaye ni mwana wa Mfalme Sobhuza, anayeendeleza ukandamizaji dhidi ya upinzani na ameisukuma nchi katika mgogoro mkubwa wa kiuchumi. Je, kuna njia yoyote inayoweza kuiondoa Eswatini katika makucha ya ufalme wa kiimla? Ni swali lililojiuliza gazeti la Die Tageszeitung, na katika kujaribu kulijibu, askofu Jose Luis Ponce de Leon wa dayosisi ya Manzini anaonyesha mashaka makubwa.

Askofu huyo anasema hakufikiria kama ungefika wakati Eswatini iwe nchi ambapo wapinzani wanauawa, akimaanisha Thulani Maseko, mwanasheria na mwanaharakati wa demokrasia ambaye aliuawa kwa bunduki na mtu asiyejulikana tarehe 21 Januari mwaka huu, akiwa na umri wa miaka 52. Kiongozi huyo wa kanisa alisema kilicho dhahiri ni kuwa mtu aliyemuuwa Maseko mbele ya familia yake ni muuaji mwenye mafunzo, sio mhalifu wa kawaida. Kushukiwa kwa ufalme kuhusika katika mauaji yake, kumezidisha mivutano.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW