Masuala ya uhamiaji ni kizungumkuti kwa Umoja wa Ulaya
25 Juni 2018Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Federica Mogherini amezihimiza nchi wanachama wa umoja huo kuweka fedha zaidi kwenye mfuko maalum kwa ajili ya Afrika wakati ambapo Umoja huo unaazimia kuanzisha vituo vya kuwachunguza wageni nje ya bara la Ulaya. Bibi Mogherini amesema mfuko huo ni muhimu na utaleta matokeo mazuri na ndio sababu ya kuomba fedha zaidi kutoka kwa nchi wanachama. Viongozi wa Umoja wa Ulaya wanatarajiwa baadaye wiki hii kupitihsa mipango itakayowawezesha wahamiaji kupata stahiki ya kuomba hifadhi katika vituo kwenye nchi za Misri, Libya, Morocco, Niger, Tunisia na Algeria.
Mpango huo mpya unafuatia makubaliano yaliyofikiwa mwaka 2015 kati ya Umoja wa Ulaya na Uturuki uliokuwa na lengo la kuihamasisha Uturuki kuwazuia wakimbizi waliotaka kwenda kwenye visiwa vya Ugiriki na umegharimu zaidi ya Euro bilioni tatu.
Wakati huohuo Algeria imelaumiwa kwa kuwatelekeza wahamiaji wapatao 13,000 katika miezi 14 iliyopita miongoni mwao wanawake waja wazito na watoto. Mamia ya wahamiaji walionusurika wanakabiliwa na mateso kwenye eneo la jangwa la Sahara. Watu hao hawana chakula au maji, wanalazimishwa kutembea kwenye jua kali na joto linalofikia nyuzi 48 Celsius wakati mwingine chini ya mtutu wa bunduki.
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amesema umoja wa Ulaya umeshindwa kupata suluhisho la pamoja kuhusiana na masuala ya uhamiaji. Ufaransa nayo inapinga mazungumzo ya Balkan licha ya Umoja wa Ulaya kuweka mlango wa wazi wake kutokana na hofu hihyo hiyo ya uhamiaji.
Chama cha siasa kali za mrengo wa kulia kinachotawala nchini Italia kilipata ushindi katika uchaguzi wa serikali za mitaa mwishoni mwa wiki, ishara kwamba kinazidi kuimarika na kuungwa mkono kutokana na sera zake za kupinga wahamiaji kutoka bara la Afrika. Vyama vinavyounda serikali ya mseto nchini Italia vya League na 5 Star vimeushauri Umoja wa Ulaya kurekebisha sera yake juu ya wahamiaji wanaotafuta hifadhi.
Kiongozi wa chama cha League Matteo Salvini ambaye pia ni waziri wa mambo ya ndani wa Italia amekwenda nchini Libya kuzungumza na viongozi wa nchi hiyo juu ya masuala ya uhamiaji. Salvini atakutana na waziri wa Mambo ya Nje wa Libya Mohamed Taher Siala na waziri mkuu Fayez Seraj na baadae viongozi hao watazungumza na vyombo vya habari.
Mwandishi:Zainab Aziz
Mhariri: Iddi Ssessanga