1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maswali ya kisheria yanayozingira uchaguzi uliorudiwa Kenya

29 Oktoba 2017

Maswali kuhusu kuaminika kwa uchaguzi huo uliosusiwa na watu wengi huenda yasimpe Rais Kenyatta ushindi wa moja kwa moja na huenda yakasababisha kesi kadhaa kuwasilishwa mahakamani

Kenia Wahlwiederholung Uhuru Kenyatta
Picha: Reuters/S. Modola

Uchaguzi mpya wa rais nchini Kenya, uliofanyika baada ya uchaguzi wa Agosti nane kubatilishwa, haujakamilika baada ya machafuko kuzuia upigaji kura katika maeneo ambayo ni ngome za upinzani. Maswali tata yangali yanasalia.

Tume huru ya uchaguzi na mipaka IEBC ingali inahesabu na kuhakiki matokeo na haijasema ni lini matokeo ya mwisho yatakapotangazwa. Tatizo kubwa ni kuwa uchaguzi haukufanywa katika majimbo manne kati ya majimbo 47 ya Kenya. Yote yako magharibi mwa Kenya, Siaya, Migori, Homa Bay na Kisumu. Maandamano yalitokea katika maeneo hayo ambayo ni ngome ya kiongozi wa upinzani Raila Odinga siku ya uchaguzi, baada ya  Odinga kuwataka wafuasi wake kutopiga kura.

Waandamanaji walizuia kufunguliwa kwa vituo vya kupiga kura, huku wakikabiliana na maafisa wa polisi. Hali hiyo ya ukosefu wa usalama iliwalazimisha maafisa wa uchaguzi kuhofia usalama wao na kukosa kusimamia uchaguzi. IEBC imesema zaidi ya vituo 3,600 kati ya vituo 40,883 havikufunguliwa.

Picha: picture-alliance/dpa

Awali IEBC iliahirisha uchaguzi katika vituo hivyo kufanywa Jumamosi, lakini ikaahirisha tena kwa muda usiojulikana.

Chini ya sheria ya Kenya, tume ya uchaguzi inaweza kutangaza matokeo endapo itahisi kuwa matokeo jumla hayataathiriwa na vituo ambavyo havijashiriki. Hata hivyo, baadhi ya wachambuzi wananyoosha kidole kwa kipengee cha katiba kinachosema uchaguzi sharti ufanywe katika maeneo yote ya uwakilishi, hali inayoiweka IEBC katika uwezekano wa kukabiliwa na kesi mahakamani endapo uchaguzi hautafanywa.

Matokeo ya uchaguzi sharti yatangazwe ndani ya siku saba baada ya uchaguzi kufanyika, ambayo itakuwa kabla ya saa sita tarehe mbiliNovemba.

Mahakama ya Juu iliubatilisha uchaguzi wa rais wa Agosti nane ambapo Uhuru Kenyatta alishinda kwa asilimia 54 huku Raila Odinga akipata asilimia 44.7, kwa misingi ya kutofuata taratibu katika kuwasilisha matokeo kielektroniki. Huo ndio ulikuwa ushindi wa kwanza wa rais kubatilishwa barani Afrika.

Baadhi ya masuali yanayoibuka

Picha: picture-alliance/AP Images/S.Abdul Azim

Maswali kuhusu kuaminika kwa uchaguzi huo uliosusiwa na watu wengi huenda yasimpe Rais Kenyatta ushindi wa moja kwa moja na huenda yakasababisha kesi kadhaa kuwasilishwa mahakamani. Kesi moja tu huenda ikazua tena hali ya sintofahamu.

Siku moja kabla ya uchaguzi huo mpya, kesi iliwasilishwa katika mahakama ya juu. Hata hivyo ukosefu wa idadi ya kutosha ya majaji wa kuisikiliza kesi hiyo ulisababisha kesi kuendelea hali iliyowashangaza waangalizi wa kimataifa na washirika wa kimataifa wa Kenya. 

Upinzani ulitaja hali hiyo kuwa njama na kuwa jaji mkuu David Maraga akalazimika kuiahirisha kesi hiyo hadi siku nyingine. Naibu wake hakuweza kuhudhuria baada ya mlinzi wake kupigwa risasi na kujeruhiwa mkesha wa siku ya uchaguzi, hali iliyoibua maswali kuhusu usalama wa maafisa wakuu na pia ikiwa majaji watashirikiana katika kesi zijazo.

Baada ya uamuzi wa kihistoria wa Septemba 1, Kenyatta aliwakashifu majaji kwa kuwaita wakora na akaahidi kuishughulikia idara ya mahakama endapo atachaguliwa tena.

Taharuki na machafuko

Picha: Reuters

Hali ya taharuki imeendelea kuyakumba baadhi ya maeneo nchini Kenya, baada ya usiku wa machafuko siku ya Ijumaa ambayo wakaazi walielezea kuwa yamechukua mkondo wa kikabila.

Machafuko hayo yamehusishwa na uchaguzi tata uliorudiwa wa rais ambao ulisusiwa na kiongozi wa upinzani Raila Odinga na ambao wapiga kura wachache ndio walijitokeza kushiriki ikilinganishwa na uchaguzi uliobatilishwa wa Agosti nane. Polisi imeshikilia kuwa watu wanne wameuawa tangu siku ya uchaguzi huo na 19 kujeruhiwa miongoni mwao maafisa 6 wa polisi.

Japo hali ya utulivu ilirejea katika maeneo kadhaa Jumamosi, polisi walitumia gesi ya kutoa machozi kuwatawanya waandamanaji katika mtaa wa mabanda wa Kawangware mjini Nairobi. Shirika la Msalaba mwekundu limetoa wito wa kuchangisha damu kuwasaidia waliojeruhiwa hasa miji ya Kisumu na Migori.

Tume inayosimamia uchaguzi Kenya IEBC inatarajiwa kutoa mwelekeo leo kuhusu shughuli ya kupiga kura katika maeneo ambayo uchaguzi uliahirishwa kufuatia ghasia. Hadi sasa, matokeo ya kura yanaonesha Rais Uhuru Kenyatta akiongoza kwa asilimia 98 ya kura.

Mwandishi: John Juma/AFPE/DPAE

Mhariri: Caro Robi

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW