Maswali yazuka kuhusu shambulizi la shule Uganda
19 Juni 2023Huku baadhi ya maafisa wa wilaya wakielezea kuwa mauaji hayo yalifanywa na kundi la waasi la ADF, tamko la waziri wa elimu kwamba huenda yalitokana na mzozo wa umiliki wa shule hiyo linaibua maswali kadhaa bila majibu.
Soma pia: Uganda yajiandaa kuwazika wahanga wa shambulizi la ADF
Kisa cha mkesha wa Jumamosi ambapo wanafunzi waliuawa kwa kuchomwa moto wakiwa katika bweni, kudungwa visu na pia kupigwa kimeleta majonzi makubwa si tu kwa wakaazi wa mji wa mpakani wa Mpondwe lakini pia kwa taifa lote la Uganda. Wanafunzi wa kiume walitetekezwa katika bweni kwa bomu la petrol huku baadhi ya wasichana wakichukuliwa mateka kubeba chakula kilichoibwa.Kulingana na majirani wa shule hiyo pamoja na jamaa za waliouawa, mauaji hayo kwenye shule ya sekodari ya Lhubiriha, yamkini uvamizi huo ulipangwa kwa muda wa siku kadhaa.
Jamaa za askari mlinzi wa shule hiyo aliyekuwa wa kwanza kuviziwa na watu hao wamo katika kuomboleza.
Kulingana na taarifa za awali, waasi wa ADF wamehusishwa na mauaji hayo kama ambavyo wamekuwa wakiyatenda katika nchi jirani ya Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo. Operesheni ya pamoja kati ya Uganda na Congo ijulikanayo kama kutokomeza waasi hao imedumu kwa miezi 18 sasa na palikuwa na matarajio kuwa ADF hawana uwezo tena kuvuka mpaka na kuingia Uganda. Hii ni kwa mujibu wa matamshi ya rais Yoweri Museveni ya mara kwa mara kuwa waasi hao wamekwisha malizwa.
Ila katika kikao cha wanahabari alichoitisha jana Jumapili ,mke wa rais Janet Museveni ambaye pia ni waziri wa elimu amejitokeza na dhana nyingine kwamba mauaji hayo yalipangwa na kufanyika kutokana na mzozo wa umiliki wa shule hiyo. Inadaiwa kuwa shule hiyo ilijengwa na misani kutoka Canada na kwa muda mrefu kumekuwa na mzozo kuhusu usimamizi na umiliki wake.
Vikosi zaidi vya wanajeshi vimepelekwa eneo hilo na kuanza kuwasaka waliotenda mauaji hayo ambao inadaiwa walitorokea misitu ya mbuga za wanyama za virunga. Wanafunzi 16 hawajulikani kule waliko na inashukiwa ni miongoni mwa waliochukuliwa mateka.