1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mataifa 14 ya Afrika yaanza biashara huria

25 Julai 2024

Mataifa 14 ya kanda ya kusini, mashariki, kati na kaskazini mwa Afrika yameanza kutekeleza mpango wa eneo huru la kibiashara miongoni mwao kuanzia Alhamis tarehe 25 mwezi Julai.

Bandari ya Djibouti
Bandari ya DjiboutiPicha: YASUYOSHI CHIBA/AFP

Hii ni baada ya jumuiya tatu za kiuchumi za COMESA, SADC na ya Afrika Mashariki kutia saini itifaki ya kuondoa vizingiti vya kibiashara baina ya mataifa wanachama 29.

Wachambuzi wa masuala ya biashara na uchumi wamesema hatua hii ni muhimu katika kutanua fursa za ajira na biashara miongoni mwa nchi hizo. Wamezihimiza nchi kama vile Tanzania na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ambazo bado zimesita kusaini itifaki hiyo kuzingatia manufaa ya soko hilo pana kwa bidhaa na huduma zao.

Kupungua kwa gharama za kufanya biashara

Kati ya mataifa 29 yaliyo katika jumuiya hizo za kiuchumi ni mataifa14 yaliyokwisha saini itifaki ya soko huru ambayo ilipitishwa mwaka 2015. Huku mengine yakiwa katika mchakato wa kujiunga kwa lengo la kurahisisha biashara miongoni mwa mataifa ya kanda hiyo kuanzia Afrika Kusini hadi Misri.

Mkutano wa kilele wa COMESA Addis AbabaPicha: Minasse Wondimu Hailu/AA/picture alliance

Wadau wameelezea kuwa jambo la muhimu ni kwamba sasa gharama za kuendesha biashara katika kanda hiyo zitapungua na hivyo kuwachochea wawekezaji wa kigeni na mashirika ya kifedha kutoa mitaji kwa njia ya mikopo.

Adrian Njau ni kaimu mkurugenzi mtendaji wa barazala wafanyabiashara wa Afrika Mashariki EABC.

"Imekuwa safari ndefu kufikia hapa. Tuna matumaini hali ya kibiashara itaboreka lakini hili linafaa kwenda sambamba na uboreshaji wa miundombinu ili kupunguza gharaza za kusafirisha bidhaa kanda hii," alisema Njau.

Kuanzishwa kwa eneo hilo huru la kibiashara kunatazamiwa pia kuzidisha biashara miongoni mwa mataifa ya bara Afrika.

Kwa sasa mataifa mengi hufanya biashara zaidi na mataifa yaliyo nje ya bara la Afrika kutokana na vizingiti vingi visivyo vya kiushuru maarufu kama NTBs. Vizingiti hivyo mara nyingi husababisha bei za bidhaa zinazozalishwa barani Afrika kuwa za juu ikilinganishwa na zile zinazotoka kwenye mataifa ya kigeni.

Furaha na hofu kwa wakati mmoja

Kuanza kutekelezwa kwa mpango huo wa eneo huru la kibiashara, kunaamabatana na kuondolewa asilimia 93 ya vizigiti hivyo hatua inayoleta matumaini ya kuimarika biashara katika kanda hiyo kuanzia leo.

Wakulima wakivuna mazao yao UgandaPicha: LUIS TATO/FAO/AFP

Umar Mzamil afisa wa masuala ya sera za biashara katika shirikisho la wenye viwanda nchini Uganda UMA ametoa angalizo hili.

"Hatua hii ni hali mseto wa furaha na hofu. Ndiyo fursa za soko pana zipo lakini vizingiti hivyo mara nyingi hujitokeza tena kutokana na ushindani na jaribio la taifa moja kjaribu kulinda maslahi ya uchumi wake," alisema Mzamil.

Naye Adrian Njau wa EABC yenye makao yake makuu Arusha anaongeza.

"Wadau kutoka sekta binafsi wanaendelezea kuwasilisha maombi kwamba mara vizingiti vikiondolewa nchi wanachama waheshimu usawazishaji wa sera za kibiashara na viwango vya kodi," Alisema Njau.

Mataifa ambayo hii leo yameanza kunufaika na mpango huo wa eneo huru la kibiashara ni Botswana, Burundi, Misri, Eswatini, Kenya, Namibia, Rwanda, Uganda, Africa Kusini, Zambia, Malawi, Lesotho, na Angola.