1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIsrael

Blinken azungumza na Abbas juu ya kuundwa taifa la Palestina

10 Januari 2024

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken amezungumza na Rais wa Mamlaka ya Palestina Mahmoud Abbas juu ya mageuzi kwenye serikali ya mamlaka ya ndani ya Wapalestinana hatua za kuundwa kwa taifa la Palestina.

Ramallah | Ziara ya Waziri wa Mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken
Waziri wa Mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken akikutana na Rais wa Mamlaka ya Palestina Mahmoud Abbas katika mji wa Muqata'a, Ramallah kwa mazungumzoPicha: Evelyn Hockstein/REUTERS

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken amefanya mazungumzo na Rais wa Mamlaka ya Palestina Mahmoud Abbas  ikiwa ni sehemu ya juhudi za Marekani za kuhamasisha mipango ya utawala wa eneo hilo baada ya vita kumalizika katika Ukanda wa Gaza, itakayojumuisha hatua madhubuti kuelekea taifa la Palestina.

Blinken amesema amehakikishiwa na mataifa kadhaa kwenye ukanda huo kusaidia ujenzi mpya na utawala wa Gaza baada ya vita vya Israel dhidi ya kundi la Hamas.

Kwenye mkutano wao mchana wa leo uliofanyika katika jiji la Ramallah huko Ukingo wa Magharibi, Blinken amemwambia Abbas kwamba Marekani inaunga mkono hatua muhimu kuelekea kuundwa kwa taifa la Palestina, hii ikiwa ni kulingana na msemaji wa Wizara ya mambo ya nje ya Marekani Matthew Miller. Amesema viongozi hao walijadiliana kwa kina juu ya mageuzi ya kiutawala.

Maono ya Blinken yanakabiliwa na kizingiti

Miller aidha amesema walizungumzia juhudi za Marekani za kushughulikia machafuko ya watu wenye misimamo mikali katika eneo la Ukingo wa Magharibi na namna ya kupunguza madhila yanayowakumba raia wa Gaza.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken akisalimiana na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu wakati alipozuru taifa hilo kwa mara ya tatu tangu kuzuka kwa vita vya israel dhidi ya HamasPicha: Antony Blinken Office/ZUMA Wire/IMAGO

Hata hivyo maono haya yaliyoainishwa na Blinken yanakabiliwa na kizingiti kikubwa, kwa kuwa serikali ya Waziri Mkuu wa Israel Benjamin inapinga vikali kuanzishwa taifa la Palestina pamoja na Israel. Mazungumzo juu ya utawala wa Palestina yamesimama licha ya Oslo ya miaka ya 1990.

Aidha, Blinken ameitaka Israeli kuikabidhi Mamlaka ya Palestina mapato yote ya ushuru iliyoyakusanya, kama walivyokubaliana, amesema Miller. Israel kwa muda mrefu imezuia sehemu ya mapato hayo ikidai kuyatumia kuwalipa wafungwa wa Palestina na kwenye vita dhidi ya Hamas.

soma pia: Blinken aona fursa kwa Israel kushirikishwa kikanda

Waandamanaji wapinga ziara ya Blinken, Ramallah

Mwanadiplomasia huyo wa ngazi za juu alipokelewa na mabango ya waandamanaji huko Ramallah, licha ya ulinzi mkali. Waandamanaji hao waolikabiliana na polisi walisema wanapeleka ujumbe wa wazi kwa Rais Abbas kutokukutana na Blinken.

Picha ikionyesha moshi ukifuka katika mji wa Khan Younis kusini mwa Ukanda wa Gaza, ambako Israel inaendeleza mashambulizi, Januari 10, 2024Picha: AFP/Getty Images

Katika ziara yake hii ya nne ya kikanda tangu kuzuka kwa vita vya Israel dhidi ya Hamas miezi mitatu iliyopita, Blinken amekutana na viongozi wa Saudi Arabia , Jordan, Qatar, Uturuki na Umoja wa Falme za Kiarabu na kusema wote hao wameonyesha kuunga mkono mipango hiyo ya baada ya vita.

Lakini hata hivyo, vita hivi  havionyeshi hata dalili ya kumalizika na kuchochea zaidi janga la kibinaadamu huko Gaza na machafuko kati ya Israel na wanamgambo wa Hezbollah wa Lebanon hivyo kuibua wasiwasi wa mzozo kusambaa.

Jioni hii Blinken amewasili Bahrain katika ziara ya ghafla, ambapo atakutana na Mfalme Hamad bin Isa Al Khalifa. Anatarajiwa pia kukutana na Mfalme Abdullah II wa Jordan na Rais wa Misri Abdel Fattah al-Sissi kuzungumzia kuongeza shinikizo la usitishwaji wa mapigano.

Taarifa kutoka Cairo, zinasema ujumbe wa Israel umewasili jijini humo leo kwa ajili ya awamu mpya ya mazungumzo na Misri kuhusiana na uwezekano wa kubadilishana mateka wanaoshikiliwa na Hamas na badala yake iwaachilie Wapalestina wanaozuiwa nchini Israel. Misri, Qatar na Marekani zimekuwa zikisimama kama wasuluhishi kati ya Israel na Hamas waliotawala Gaza kwa karibu miaka 17.

Wizara ya Afya ya Gaza imesema hii leo kwamba karibu watu 23,357 wameuawa kutokana na vita kwenye eneo hilo.

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi
Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW