1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uhispania, Senegal zazindua muungano dhidi ya ukame

8 Novemba 2022

Mataifa yaliokumbwa na ukame, yakiongozwa na Senegal na Uhispania, yametangaza muungano kusaidiana kudhibiti uhaba wa maji kwa kubadilishana teknolojia na utaalamu. Uzinduzi huo umefanyika kandoni mwa mkutano wa COP27.

Indien Dürre in Jharkhand
Picha: Altaf Qadri/AP Photo/picture alliance

Tangazo hilo lilitolewa kandoni mwa mkutano wa mazingira wa Umoja wa Mataifa, COP27, unaofanyika nchini Misri, baada ya kukosekana mvua kwa msimu wa tano mfululizo katika kanda ya pembe ya Afrika.

Akihutubia wawakilishi wa muungano huo, gavana wa Kaunti ya Embu nchini Kenya Cecily Mbarire, alisema nchi yake inashuhudia ukame mbaya zaidi katika kipindi cha miaka 40.

Soma pia: Guterres:Tuchukue hatua za pamoja ama tuangamie sote

Watabiri wa hali ya hewa wameonya juu ya uwezekano wa msimu usiokifani wa sita wa kukosekana kwa mvua mwaka ujao.

"Tumekuwa na misimu minne mfululizo bila mvua na kuna matarajio makubwa ya msimu wa sasa mfupi wa mvua kuwa wa tano," alisema gavana Mbarire.

"Kimsingi tunashuhudia ukame mbaya zaidi katika miaka 40 kama taifa."

Mkutano wa kilele wa Tabianchi, COP27 waanza Misri

02:30

This browser does not support the video element.

Waziri mkuu wa Uhispania Pedro Sanchez, alisema ukame umekuwa na madhara yasiokifani, wakati wa uzinduzi wa muungano huo ambapo nchi yake inapanga kuchagia kiasi cha dola milioni tano katika mwaka wa kwanza.

Soma pia: Mkutano wa COP27 waanza kwa onyo Misri

Sanchez alisema mwaka huu Ulaya imeshuhudia ukame mbaya zaidi katika kipindi cha miaka 500, na Afrika na kanda nyingine za dunia zinakumbwa pia na uhaba mkali wa maji.

Ukame waongezeka kwa asilimia 29

Kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa lenye dhamana ya kuzuwia kuenea kwa jangwa, UNCCD, ukame umezidi kuikumba dunia kwa asilimia 29 tangu mwaka 2000, wakati ambapo joto likichochea ukataji misitu na usimamizi duni wa ardhi katika kukausha maeneo yaliokuwa na hali ya wastani hapo kabla.

Soma piaRais Samia: Matumizi ya kuni na mkaa chanzo cha ukame

Naibu Katibu Mtendaji wa UNCCD, Andrea Meza, anasema maandalizi zaidi yanahitajika kwa ajili ukame ujao.

"Tunachojua na inachotuambia sayansi ni kwamba tutakuwa na matukio zaidi ya ukame, makubwa na ya kujirudia na tuhahitaji kujiandaa," alisema Meza.

Aliongeza kuwa dunia inahitaji kubadilisha mtazamo wake. "Tunahitaji kujiandaa kwa ajili ya ukame ujao."

Wanasayansi wanasema ukame utakuwa mbaya zaidi na wa kujirudia katika miaka ijayo, na pia utadumu muda mrefu zaidi mnamo wake joto la dunia likivuruga miendeneo ya hali ya hewa.

Wanasayansi wameonya kuwa ukame na majanga mengine yatokanakayo na mabadiliko ya tabianchi vitaongezeka na kujirudia rudia katika miaka ijayo.Picha: DW

Majanga kuigharimu dunia zaidi ya dola trilioni 5

Ripoti iliyotolewa mwezi Agosti na shirika la ushauri wa uhandisi wa kimazingira GDH, ilionyesha kuwa kufikia mwaka 2050, usumbufu wa hali ya hewa, ikiwemo ukame pamoja na upepo mkubwa na mvua, huenda vikaugharimu uchumi wa dunia dola trilioni 5.6.

Soma pia: Nusu ya nchi duniani hazina mifumo ya tahadhari ya majanga

Meza amesema hakuna nchi ina kinga dhidi ya ukame, na watu walioathirika vibaya zaidi hawaezi kuzalisha chakula, umeme au kufanya biashara wakati mito ikikauka, na kuzuwia usafirishaji.

Kwa mujibu wa waziri mkuu wa Uhispania, Pedro Sanchez, muungano huo unaoshirikisha mataifa 25 na mashirika yapatayo 20, utalenga kuhamasisha rasilimali kupambana na ukame pale utakapojitokeza, lakini hakutoa ufafanuzi kuhusu kiasi gani cha pesa kinaweza kutengwa.

Chanzo: mashirika