Mataifa makubwa yakubali mpango wa mpito Syria
1 Julai 2012Urusi na China zimesisitiza kuwa Wasyria wanapaswa kuamua juu ya vipi kipindi hicho cha mpito kitafanyika badala ya kuruhusu watu wengine kuamua hatima ya nchi hiyo kwa niaba yao, wakati mataifa hayo mawili yenye ushawishi mkubwa yakitia saini makubaliano ya mwisho ambayo hayakutoa wito wowote wa moja kwa moja kwa Assad kuachia madaraka.
Makubaliano hayo yamekuja licha ya shaka shaka za mwanzo kutoka kwa washiriki juu ya uwezekano wac mazungumzo ya Geneva huku kukiwa na mgawanyiko mkubwa kati ya mataifa ya magharibi kwa upande mmoja na China na Urusi kwa upande mwingine juu ya kumaliza kwa ghasia na matumzi ya nguvu ambayo yamesababisha kiasi watu 83 kupoteza maisha siku ya Jumamosi.
Wachunguzi wa haki za binadamu wamesema kuwa wengi wa wahanga ni raia na mamia zaidi ya watu wengine wamekwama katika mji wa Douma wakati majeshi ya serikali yalipovamia mji huo katika jimbo la Damascus.
Serikali ya mpito
Wakati mjumbe wa kimataifa kwa ajili ya Syria Kofi Annan hakutaja majina na kusema ni juu ya Wasyria wenyewe kuamua nani wanamtaka awemo katika serikali hiyo ya umoja wa kitaifa , ameongeza. Nitashangaa kuwa Wasyria , watachagua watu ambao wana damu mikononi mwao.
Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Hillary Clinton ameweka wazi kuwa Marekani haioni Assad kuwa atakuwa na nafasi ya uongozi katika kipindi hicho cha mpito.
Assad lazima aondoke
Assad ni lazima aondoke. Hawezi kufaulu mtihani wa ridhaa ya pamoja , amesema.
Waziri wa mambo ya kigeni wa Ufaransa Laurent Fabius alikuwa na msimamo kama huo , akisema, "Ni dhahiri kuwa Assad lazima aondoke".
Hakuna mtu anayeweza kudhania kwa dakika moja kuwa Assad atakuwamo katika serikali mpya, kama vile mtu anavyoweza kufikiria kuwa kuna uwezekano wa yeye kuunda mazingira yatakayokuwa hayaelemei upande wowote, kama inavyotakiwa na makubaliano hayo, amesema waziri huyo na kuongeza kuwa serikali ya mpito , itawaengua wauwaji.
Waziri wa mambo ya kigeni wa Uingereza William Hague amekiri kuwa makubaliano hayo ni makubaliano ya muafaka, wakati Urusi ilichukua msimamo kuwa imeyashawishi mataifa mengine makubwa duniani kuwa haitakubalika kuyatenga makundi yoyote katika hatua hiyo ya mpito.
Urusi yamkingia kifua Assad
Urusi ikiwa ni mshirika wa muda mrefu wa Syria , inajisikia vibaya kumuweka kando Assad, hata kama mahusiano kati ya Urusi na Syria yameanza kupooza.
Waziri wa mambo ya kigeni wa Urusi Sergei Lavrov amesema ," Ni vipi hasa kazi ya mpito itafanyika kuelekea katika hatua mpya itaamuliwa na Wasyria wenyewe".
Mwandishi : Sekione Kitojo /afpe
Mhariri : Sudi Mnette