1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
UtandawaziKimataifa

EU, China na India zapinga ushuru wa Trump

26 Novemba 2026

Umoja wa Ulaya, China, India na Japan zimepinga pendekezo jipya la Marekani la kuongeza ushuru kwa bidhaa kutoka mataifa kadhaa. Hatua hiyo inaibua hofu ya mvutano mpya katika biashara ya dunia.

Marekani, Washington D.C. 2026 | Donald Trump
Mataifa makubwa yapinga ushuru mpya wa MarekaniPicha: Alex Brandon/AP Photo/picture alliance

Pendekezo jipya la Marekani la kuongeza ushuru kwa bidhaa kutoka mataifa 14, likiwemo Umoja wa Ulaya, China, India na Japan, limezua upinzani kutoka kwa washirika wake wakuu wa biashara. 

Utawala wa Rais Donald Trump unasema hatua hiyo inatokana na uchunguzi wa miezi kadhaa kuhusu kile Washington inachokiita uzalishaji uliopitiliza katika baadhi ya sekta. Viwango hivyo vipya vinapendekezwa kufikia asilimia 20 kwa baadhi ya nchi.

Umoja wa Ulaya umesema unakataa vikali madai kwamba Ulaya ni chanzo cha uzalishaji wa ziada unaopotosha biashara.

Msemaji wa Tume ya Ulaya Olof Gill amesema Brussels na Washington kwa muda mrefu zimekuwa na wasiwasi wa pamoja kuhusu uzalishaji mkubwa unaochochewa na misaada ya serikali katika nchi nyingine, hasa China.

Rais wa Marekani Donald Trump na Waziri Mkuu wa India Narendra Modi Picha: Carlos Barria/REUTERS

Hata hivyo, Umoja wa Ulaya unasema unatarajia Marekani kuheshimu makubaliano ya ushuru yaliyofikiwa mwaka 2025 ambayo yalipunguza ushuru wa Marekani kwa bidhaa za umoja huo hadi asilimia 15.

India yasema masuala ya biashara yatatuliwe kupitia mazungumzo

China nayo imekosoa vikali pendekezo hilo. Wizara ya Biashara ya China imesema kutumia hoja ya uzalishaji uliopitiliza kama msingi wa ushuru mpya ni kisingizio cha kulinda soko la ndani. He Yadong, Msemaji wa Wizara ya Biashara ya China amesema:

"China inaitaka Marekani kurekebisha kile ilichokiita hatua zisizo sahihi na kurejea katika njia ya mazungumzo na mashauriano. Pia imesema itafuatilia kwa karibu maendeleo na inahifadhi haki ya kuchukua hatua zinazofaa kulinda maslahi yake halali," alisema Yadong.

India, ambayo inapendekezewa ushuru wa asilimia 17, imesema masuala ya biashara yanapaswa kutatuliwa kupitia mazungumzo yanayoendelea ya makubaliano ya biashara baina ya nchi hizo mbili.

Kwa upande wake,Japan imesema inapinga madai kwamba ina uzalishaji uliopitiliza kimuundo, na kueleza kuwa ni jambo la kusikitisha kulengwa na ushuru huo licha ya kushirikiana na Marekani katika kushughulikia tatizo hilo katika nchi nyingine.

Wachambuzi wanaonya kuwa iwapo ushuru huo mpya utaanza kutumika baada ya kipindi cha maoni ya umma kumalizika, unaweza kuongeza gharama za biashara, kuathiri minyororo ya usambazaji duniani na kuongeza mvutano katika uchumi wa kimataifa ambao tayari unakabiliwa na changamoto za ukuaji.

 

Imehaririwa na:Saumu Mwasimba
Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW