Mataifa makubwa yataka uchaguzi wa Libya kuungwa mkono
13 Novemba 2021Viongozi wa mataifa mbalimbali waliohudhuria mkutano huo wametishia kuwawekea vikwazo vya kimataifa wale waliowataja kama wavurugaji wa uchaguzi wa rais uliopangwa kufanyika Disemba 24 nchini Libya kwenye mkutano huo kuhusu Libya uliofanyika Paris, Ufaransa.
Sehemu ya tamko la viongozi hao aidha limewatolea mwito wadau nchini Libya kuhamasisha kufanyika kwa uchaguzi huo wa rais na wabunge katika njia ya uhuru, wa haki na ambao utajumuisha pande zote.
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron alikuwa mwenyeji wa mkutano huo uliohudhuriwa na wakuu wa mataifa, serikali na mawaziri wa mambo ya kigeni, kansela wa Ujerumani Angela Merkel na makamu wa rais wa Marekani Kamala Harris. Viongozi wa Libya, Misri na Italia pia walihudhuria.
Mpango unaoungwa mkono na Umoja wa Mataifa ni wa kufanyika kwa uchaguzi mwezi ujao nchini Libya, taifa lililokumbwa na machafuko tangu vuguvugu lililosababisha kuondolewa madarakani kwa kiongozi wa muda mrefu Moammar Gadhafi mwaka 2011, ambalo pia liliungwa mkono na vikosi vya kujihami vya NATO. Umoja wa Mataifa inauchukulia mpango huo kama msingi muhimu wa kurejesha utulivu nchini Libya baada ya muongo wa machafuko na mzozo.
Urusi na Uturuki zapeleka wawakilishi wa ngazi za chini.
Urusi na Uturuki hata hivyo ambao ni wadau muhimu katika mchakato wa amani nchini Libya walipeleka wawakilishi wa ngazi ya chini licha ya mialiko ya wakuu wa mataifa hayo kwenye mkutano huo. Uturuki ina wasiwasi kwamba Ufaransa huenda ikataka kuondoka kwa majeshi yake nchini Libya, ambayo inadai kwamba ni ya kawaida na yalialikwa na serikali inayotambuliwa na Umoja wa Mataifa, tofauti na wanajeshi kutoka mataifa mengine.
Urusi ina mamluki wake wanaosaidiana na vikosi vya Libyan National Army vilivyojikita mashariki mwa nchi hiyo na vinavyosaidiwa na Umoja wa Falme za Kiarabu na Misri.
Jana Ijumaa, rais Macron aliuambia mkutano huo kwamba Urusi na Uturuki wanatakiwa kuutekeleza mpango wa kuwaondoa mamluki wao.
Zikiwa zimesalia wiki sita hadi kufanyika kwa uchaguzi huo, mvutano bado unaendelea kushuhudiwa miongoni mwa pande zinazohasimiana, serikali inayotambuliwa na Umoja wa Mataifa iliyoko mashariki, vikosi vinavyomtii mbabe wa kivita Khalifa Haftar vilivyoko upande wa magharibi na pande nyingine za kisiasa.
Miongoni mwa masuala makubwa yanayozozaniwa ni kanuni zinazohusiana na ratiba ya uchaguzi na nani hasa anayeruhusiwa kushiriki kwenye mchakato huo.
Kuna hofu pia kuhusiana na iwapo pande hizo hasimu zitayakubali matokeo ya uchaguzi jambo ambalo linaweza kuamua mustakabali wa nchi hiyo ambayo pia imekuwa kituo kikuu cha kuwasafirisha wahamiaji wanaopania kuvuka bahari ya Mediterenia na kuingia Ulaya.
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametuma ujumbe wa video kwenye mkutano huo akionya kwamba yoyote atakayehusika na kuhujumu mchakato wa amani nchini Libya atawajibishwa.
Mashirika: DW